Wasiwasi wa machafuko na ukosefu wa amani ungalipo mashariki mwa DRC
Mjumbe wa Kamisheni ya Uadilifu na Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameelezea wasiwasi mkubwa alionao kutokana na kuongezeka machafuko na ukosefu wa amani katika mji wa Bukavu ambao ni makao makuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini.
Justin Nkunzi, Mjumbe wa Kamisheni ya Uadilifu na Amani amesema kuwa, kuongezeka vitendo vya wizi wa kutumia silaha na mauaji dhidi ya raia katika wiki za hivi karibuni kumeufanya mji huo kutawaliwa na mazingira yasiyo na usalama.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, vijana wawili wamemuua kasisi mmoja akiwa katika eneo lake la kazi mjini Bukavu. Ukosefu wa amani katika mji wa Bukavu ulioko katika mkoa wa Kivu Kaskazini umezusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa raia pamoja na jumuiya za kiraia.
Maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa yakishuhudia machafuko na ukosefu wa amani kwa zaidi ya miongo miwili sasa. Hali hiyo imewafanya raia wengi kuyakimbia makazi yao na kuomba hifadhi ya ukimbizi katika nchi jirani.
Kutokuwa na uwezo jeshi la nchi hiyo na kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa MONUSCO wa kuyasambaratisha makundi ya waasi yanayoendesha harakati zao katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo kumesababisha usalama na amani uzidi kukosekana katika maeneo hayo.
Makundi kadhaa ya waasi kutoka Rwanda na Uganda yamekuwa yakiendesha shughuli zao katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.