Kongo kupeleka walinzi katika maeneo ya migodi ili kuzuia wizi wa madini
-
Kongo kulinda madini yake
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, katika jitihada za kuzuia uporaji wa madini yake, imetangaza mpango wa kupeleka kikosi maalumu cha wanamgambo kitakachokuwa na jukumu la kulinda sekta ya madini nchini humo.
Katika taarifa yake, Mkaguzi Mkuu wa Madini wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema kuwa kitengo hicho kinachojulikana kama "Mlinzi wa Madini" kitakuwa na jukumu la kuhakikisha usalama katika mnyororo mzima wa uchimbaji madini, ikiwa ni pamoja na ulinzi wa maeneo ya uchimbaji na usafirishaji salama wa madini kutoka maeneo ya uchimbaji hadi vituo vya usindikaji na mipakani.
Serikali ya Kinshasa imesema kuwa uwekezaji wa awali wa takriban dola milioni 100 umetengwa kwa lengo la kugharamia mafunzo ya miezi sita kwa waajiri pamoja na vitendea kazi.
"Kikosi cha kwanza cha mawakala 2,500 hadi 3,000 kinatarajiwa kutumwa katika mikoa 22 nchini Jamuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na mafunzo yao yamepangwa kuanzia Juni hadi Desemba", imeeleza taarifa ya serikali.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, rasilimali nyingi za madini ya Kongo zinapatikana mashariki mwa nchi eneo ambalo limeathiriwa na hali ya ukosefu wa amani kwa muda mrefu sasa.
Utajiri huo wa madini umepelekea kuibuka mapigano kati ya makundi ya wanamgambo wenye silaha.