Yahya Jammeh kukabidhi madaraka mwezi Januari
Yahya Jammeh Rais wa Gambia aliyeangushwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika hivi karibuni nchini humo angali yupo nchini humo na atakabidhi madaraka kwa rais mteule, Adama Barrow mwezi Januari mwakani. Hayo yameelezwa na Waziri wa Mawasiliano wa Gambia.
Jammeh ambaye amekuwa madarakani nchini Gambia kwa kipindi cha miaka 22 hajaonekana hadharani tangu alipowashangaza waangalizi wa uchaguzi kwa kukubali kushindwa katika uchaguzi huo wa Rais uliofanyika Disemba Mosi.
Kitendo cha kutoonekana hadharani Yahya Jammeh kimeibua tetesi kuwa kiongozi huyo ameikimbia nchi.
Kuangushwa Jammeh katika kinyang'anyiro hicho cha uchaguzi wa Rais kulipokelewa kwa sherehe na shangwe kubwa za wananchi mwishoni mwa wiki.
Taarifa ya Waziri wa Mawasiliano wa Gambia imesisitiza kuwa, Yahya Jammeh bado yupo katika makazi yake ikulu na atakutana na Adama Barrow, Rais Mteule wa Gambia wiki ijayo.
baada ya kuchaguliwa na wananchi wa Gambia, Adama Barrow, alisema atatengue uamuzi wa mtangulizi wake Yahya Jammeh wa kuiondoa nchi hiyo katika Mkataba wa Roma uliobuni Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC. Amesisitiza kuwa, lengo la ICC ni kuhimiza utawala bora duniani jambo ambalo binafsi analiamini.