Viongozi wa Nigeria wang'ang'ania Sheikh Zakzaky afunguliwe mashtaka
Licha ya Mahakama Kuu ya Nigeria kutoa amri ya kuitaka serikali ya shirikisho imwachie huru kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky, viongozi wa jimbo la Kaduna wangali wanashikilia kiongozi huyo wa kidini ashtakiwe na kuhukumiwa kifungo jela.
Hivi karibuni Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa amri ya kuachiwa huru Sheikh Zakzaky ambaye pamoja na mkewe wanashikiliwa korokoroni kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa bila ya kufikishwa mahakamani.
Maafisa wa serikali ya jimbo la Kaduna walitangaza jana kuwa lazima Sheikh Ibrahim Zakzaky apandishwe kizimbani kwa kile walichodai "utovu wa sheria" uliofanywa na wanachama wa harakati ya Kiislamu ya Nigeria kwa muda wa miongo mitatu sasa.
Katika hatua kandamizi iliyochukua dhidi ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria serikali ya jimbo la Kaduna ilitangaza mnamo mwezi Oktoba uamuzi ya kuipiga marufuku harakati ya Kiislamu ya Nigeria. Aidha hapo jana viongozi wa jimbo hilo waliituhumu harakati hiyo kuwa ina "mfungamano na dola moja la kigeni".
Hii ni katika hali ambayo siku chache zilizopita Jaji Gabriel Kolawole wa kitengo cha Abuja cha Mahakama Kuu ya Nigeria aliiamuru serikali imwachilie huru bila ya masharti yoyote Sheikh Zakzaky na mke wake katika kipindi cha siku 45 baada ya kutolewa agizo hilo.
Katika uamuzi wake huo Jaji Kolawole aliongeza kuwa kutokana na kukiuka haki za Sheikh Zakzaky pamoja na mkewe na kutokana na wawili hao kushikiliwa kinyume cha sheria, kitengo cha huduma za usalama cha serikali kina wajibu wa kuwalipa kila mmoja fidia ya dola zipatazo 79,000.
Hata hivyo tamko la hapo jana la maafisa wa serikali ya jimbo la Kaduna dhidi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky linaweza kutatiza utekelezaji wa hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Nigeria ya kuachiwa huru mwanazuoni huyo.../