Mapigano ya kuwania maeneo ya mafuta yapamba moto Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20980-mapigano_ya_kuwania_maeneo_ya_mafuta_yapamba_moto_libya
Msemaji wa vikosi vya kulinda bandari za mafuta nchini Libya ametangaza habari ya kuongezeka mapigano karibu na taasisi muhimu za mafuta za nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 07, 2016 23:38 UTC
  • Mapigano ya kuwania maeneo ya mafuta yapamba moto Libya

Msemaji wa vikosi vya kulinda bandari za mafuta nchini Libya ametangaza habari ya kuongezeka mapigano karibu na taasisi muhimu za mafuta za nchi hiyo.

Muhammad Qabeli, msemaji wa gadi ya taasisi za mafuta za Libya alitangaza habari hiyo jana Jumatano na kuongeza kuwa, makundi ya watu wenye silaha yanafanya njama za kuzidhibiti taasisi hizo za mashariki mwa Libya na wametumia silaha nzito kuushambulia mji wa Bin Jawad kabla ya kuuteka.

Ameongeza kuwa, pamoja na hayo, vikosi vya mashariki mwa Libya viko imara kukabiliana na mashambulizi hayo na kuzilinda taasisi za mafuta katika eneo linalojulikana kwa jina la Hilal ya Mafuta.

Hilal ya Mafuta ni eneo ambalo linajumuisha bandari na vituo muhimu vya kusafirishia mafuta nchini Libya na eneo hilo lilitekwa na vikosi vya Khalifa Haftar miezi kadhaa iliyopita.

Wanajeshi wa Libya 

 

Libya haijawahi kushuhudia utulivu tangu ulipopinduliwa utawala wa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011, baada ya jeshi la nchi za Magharibi NATO kuivamia nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kufanya uharibifu mkubwa na baadaye kuitelekeza huku silaha zikiwa zimetapakaa mikononi mwa makundi yenye silaha ambayo kila moja lina hamu ya kudhibiti utajiri wa nchi hiyo.

Magenge mengine ya kigaidi kama vile Daesh nayo yametumia fursa hiyo kujipenyeza nchini Libya na kujizatiti ingawa taarifa zinasema kuwa, serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya imefanikiwa kuwafurusha magaidi hao kwenye maeneo karibu yote ya nchi hiyo.