Kenyatta: Kenya inatathmini kwa kina mpango wa kujiondoa ICC
Kwa mara nyingine tena Kenya imeweka bayana azma ya kuangalia upya uhusiano wake na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).
Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki amesema kuwa nchi hiyo inathmini kwa umakinifu mkubwa na kwa kina suala la kujiengua kwenye Mkataba wa Roma uliobuni ICC, ambapo mara mbili Bunge la kitaifa la nchi hiyo limepasisha hoja ya kujiondoa ICC, lakini hoja hiyo ikatupilia mbali kwa kutopata uungaji mkono wa kutosha.
Akihutubia taifa katika maadhimisho ya 53 ya Siku ya Jamhuri hapo jana jijini Nairobi, Rais Kenyatta alisema kuwa: "Tumefanya juhudi za kuitaka ICC ifanyie marekebisho kanuni na sheria zake, ili mahakama hiyo isikiuke uhuru wa kujitawala wa nchi, lakini hatujaona mabadiliko yoyote na hilo, linatusukuma tuangalie upya uhusiano wetu na mahakama hiyo."
Ameongeza kuwa, taasisi hiyo haina uadilifu na imekuwa ikiegemea upande mmoja katika maamuzi yake, na kwamba kama zilivyofanya baadhi ya nchi kujiondoa na nyingine kutangaza azma zao za kufuata mkondo huo, Kenya pia imeliweka kwenye mizani suala hilo.
Mwezi wa Oktoba, Gambia ilijiunga na orodha ya nchi kadhaa za Afrika zilizotangaza azma yao ya kujiondoa katika Mkataba wa Roma uliobuni ICC Julai mwaka 2002, ingawaje Rais mteule wa nchi hiyo Adama Barrow alisema kuwa ataliangalia upya suala hilo.
Tayari Afrika Kusini na Burundi zimeanzisha mchakato wa kujiondoa katika Mkataba wa Roma kutokana na kile viongozi wa nchi hizo sawa na viongozi wengine wa Kiafrika wanakitaja kuwa, ICC kuwasakama tu viongozi wa nchi za bara hilo, huku ikifumbia macho jinai zinazofanywa na viongozi wa Magharibi, huku Uganda na Namibia zikiashiria kuwa yumkini nazo zikajiunga na mkondo huo wa kujiondoa ICC.