Dec 15, 2016 06:53 UTC
  • SID: Serikali ya Jubilee nchini Kenya imeshindwa kupambana na ufisadi

Shirika la kutetea haki za umma la SID limetangaza kuwa SERIKALI ya Jubilee nchini Kenya imetimiza ahadi moja pekee kati ya 30 ilizotoa kuhusiana na mikakati ya kupambana na ufisadi.

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa (SID) jijini Nairobi, imesema kuwa ahadi pekee ambayo serikali imetimiza ni mkakati wa kutafuta na kutwaa pesa zilizoibwa. Shirika hilo lilisema serikali ya Kenya imelegea katika utekelezaji wa ahadi nyinginezo, hali ambayo imeongeza mara dufu kiwango cha ufisadi.

Bw Irungu Houghton, ambaye ni miongoni mwa wakurugenzi wa shirika hilo amesema hizo ni dalili za hali ya hatari ambazo huenda hata zikahatarisha nafasi ya Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi ujao.

Kulingana na ripoti hiyo ambayo inaangazia mikakati ya kupambana na ufisadi kati ya mwaka 2013 na 2016, baadhi ya ahadi ambazo serikali imefeli kutekeleza ni usimamizi bora wa mfumo wa IFMISS ambao inadaiwa umetumiwa na walaghai kuiba pesa za umma.

Rais Uhuru Kenyatta

Nyingine ni utoaji huduma katika sekta ya ardhi kwa njia ya dijitali na kuiwezesha Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuwashtaki wale wanaopatikana na makosa ya kushiriki katika ufisadi.

Hata hivyo, shirika hilo lilisema kuwa badala yake, serikali imekuwa ikifanya njama za kupunguza nguvu za asasi hizo, hivyo kuathiri mfumo wa kukabiliana na ufisadi.

Bw Irungu Houghton amesema kuwa kesi nyingi za ufisadi zinazowakabili mawaziri na viongozi wakuu zingali mahakamani, hali ambayo imewafanya Wakenya wengi wakate tamaa kuhusu iwapo kweli serikali imejitolea kumaliza ufisadi.

 

Tags