Mahakama Gambia kusikiza kesi ya uchaguzi Januari 10
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21904-mahakama_gambia_kusikiza_kesi_ya_uchaguzi_januari_10
Mahakama ya Kilele ya Gambia imeakhirisha hadi Januari 10 mwakani kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais iliyowasilishwa na Rais Yahya Jammeh anayetaka matokeo ya uchaguzi yabatilishwe.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Dec 22, 2016 03:26 UTC
  • Mahakama Gambia kusikiza kesi ya uchaguzi Januari 10

Mahakama ya Kilele ya Gambia imeakhirisha hadi Januari 10 mwakani kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais iliyowasilishwa na Rais Yahya Jammeh anayetaka matokeo ya uchaguzi yabatilishwe.

Mahakama hiyo ambayo mwenyekiti wake ni Jaji Mkuu Emmanuel Fagbenle imeamuru kuwa, kesi hiyo iakhirishwe kwa sababu Tume Huru ya Uchaguzi Gambia ilikuwa bado haijapokea  nyaraka za kesi.

Awali Jammeh ambaye ameiongoza Gambia kwa miaka 22 alikubali matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyompa ushindi mpinzani wake, Adama Barrow na hata kumpongeza hadharani. Hata hivyo wiki moja baadaye kiongozi huyo alitengua msimamo wake huo na kutangaza kuwa kulifanyika udanganyifu katika uchaguzi huo.

Adama Barrow

Rais Jammeh ameyakataa matokeo ya uchaguzi wa rais kwa madai ya kile alichokiita makosa yasiyokubalika yaliyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Gambia na kutaka uitishwe uchaguzi mwingine mpya.

Barrow alikuwa amepangiwa kuchukua hatamu za uongozi Januari 18 mwakani lakini sasa uamuzi wa mahakama ndio utakaoainisha hatima ya nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika.