Dec 24, 2016 04:50 UTC
  • Ecowas: Ikibidi, tutatuma askari wa kieneo nchini Gambia Januari

Viongozi wa wawakilishi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) wametishia kutuma vikosi vya kieneo nchini Gambia, iwapo Rais Yahya Jammeh atakaa kukabidhi madaraka wakati muda wake utakapiomalizika rasmi Januari 19 mwakani.

Marcel Alain de Souza, Rais wa ECOWAS jana Ijumaa aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Mali, Bamako kuwa, vikosi vya kijeshi vya eneo viko tayari kuwapa Wagambia kiongozi wao waliomchagua kwa nguvu, iwapo wapatanishi wanaoongozwa na Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari watashindwa kumshawishi Jammeh kuachia madaraka.

Viongozi wa Ecowas wakimshawishi Jammeh aachie ngazi

Amebainisha kuwa, sio azma ya jumuiya hiyo ya kieneo kuingilia kijeshi na kuchochea machafuko na ghasia katika nchi hiyo na kwamba iwapo Jammeh analipenda taifa lake, hana budi kuondoka madarakani kufikia Januari 19.

Haya yanajiri siku chache baada ya Mahakama ya Kilele ya Gambia kuakhirisha hadi Januari 10 mwakani, kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais iliyowasilishwa na Jammeh anayetaka matokeo ya uchaguzi yabatilishwe.

Hii ni katika hali ambayo, Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayemaliza muda wake, amemtaka Rais Yahya Jammeh amkabidhi madaraka kwa amani Adama Barrow mgombea wa muungano wa upinzani aliyeshinda katika uchaguzi huo. Kadhalika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba lililaani hatua ya Rais wa Gambia ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais na kumtaka aheshimu chaguo la wananchi.

Adama Barrow, mfanyabiashara aliyetangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais Gambia

Tarehe 9 mwezi huu, Yahya Jammeh  alijitokeza na kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais, wiki moja baada ya yeye binafsi kukubali kubwagwa katika kinyang'anyiro hicho na Adama Barrow mgombea kutoka muungano wa upinzani. 

Tags