20 wahofiwa kufa maji baada ya boti kuzama Ziwa Victoria, Uganda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22033-20_wahofiwa_kufa_maji_baada_ya_boti_kuzama_ziwa_victoria_uganda
Makumi ya watu wanahofiwa kupoteza maisha baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama katika Ziwa Victoria nchini Uganda.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 24, 2016 04:04 UTC
  • 20 wahofiwa kufa maji baada ya boti kuzama Ziwa Victoria, Uganda

Makumi ya watu wanahofiwa kupoteza maisha baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama katika Ziwa Victoria nchini Uganda.

Richard Musisi, Mkuu wa Wilaya ya Kalangala amesema boti hiyo ambayo ilikuwa imebeba watu 30 ilizama mwendo wa saa tano na nusu mchana jana Ijumaa, ikitokea eneo la Bukasa kuelekea Entebbe.

Amesema kufikia sasa timu ya waokoaji na wapiga mbizi imefanikiwa kuopoa miili sita toka majini huku watu wanne wakinusurika katika ajali hiyo. Inaarifiwa kuwa, Polisi ya Pwani ya Uganda iliwakataza watu hao kusafiri kutokana na wingi wao na udhaifu wa chombo chao cha usafiri, mbali na kutokuwa na mafulana maalumu ya dharura.

Ramani ya Ziwa Victoria

Hata hivyo wasafiri hao walisisitiza kuwa lazima waendelee na safari yao kwa minajili ya kwenda kujumuika na jamaa zao wakati huu wa sherehe za kufunga mwaka.

Itakumbukwa kuwa, mwaka 2010, watu zaidi ya 60 walifariki dunia baada ya feri waliyokuwa wakisafiria kuzama katika Ziwa Victoria,  nje kidogo ya bandari ndogo ya mjini Entebbe nchini Uganda.

Si vibaya kukumbusha kuwa, mwaka 1996 ajali mbaya ya aina hiyo ilitokea wakati meli iliyokuwa ikisafiri kutoka Bukoba kuelekea Mwanza ilipozama na kuua zaidi ya watu 800.