Mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa DRC yanaendelea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22057-mazungumzo_ya_kuutafutia_ufumbuzi_mgogoro_wa_drc_yanaendelea
Mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yameendelea huku wapinzani wakiendelea kushikilia msimamo wao wa kuondoka madarakani Rais Joseph Kabila.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 24, 2016 15:11 UTC
  • Mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa DRC yanaendelea

Mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yameendelea huku wapinzani wakiendelea kushikilia msimamo wao wa kuondoka madarakani Rais Joseph Kabila.

Shirika la habari la Reuters limeripoti habari hiyo na kuwanukuu washiriki wa mazungumzo hayo ya kisiasa wakisema leo Jumamosi kwamba, mazungumzo yanayoendelea baina ya wapinzani na muungano tawala yamefikia makubaliano ya kuondoka madarakani Rais Joseph Kabila mwaka 2017.

Kwa mujibu wa Reuters, mazungumzo hayo yameendelea kuwa upatanishi wa maaskofu wa Kanisa Katoliki. Kwa mujibu wa shirika hilo, mazungumzo ya leo baina ya pande hizo mbili yamesita saa 11.30 asubuhi kwa saa za DRC baada ya kupita karibu masaa 12 ya mazungumzo ya kina ya mfululizo baina ya pande hizo.

Rais Joseph Desire Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

 

Mjumbe wa upande wa upinzani, Francois Mwamba amesema, kuna baadhi ya mambo yamebakia inabidi yajadiliwe. Kwa mujibu wa Mwamba, ilitarajiwa makubaliano ya mwisho yatiwe saini leo jioni. Makubaliano hayo yatakuwa ni mafanikio makubwa kwa nchi hiyo ambayo haijawahi kushuhudia makabidhiano ya amani ya madaraka tangu ilipopata uhuru kutoka kwa mkoloni Ubelgiji mwaka 1960.

Machafuko yameongezeka huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika wiki za hivi karibuni huku wapinzani wakidai kuwa Rais Joseph Kabila anafanya njama za kujiongezea muda wa kubakia madarakani nchini humo. 

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni nchi ya nne kwa kuwa na watu wengi zaidi barani Afrika na ina utajiri mkubwa wa maliasili ambao daima unakodolewa macho ya tamaa na madola ya kigeni. 

Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakiwa katika barabara za Kinshasa kwa ajili ya kukabiliana na machafuko