Mgogoro wa kisiasa na kuongezeka ukosefu wa usalama nchini Libya
Wakati Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya akifuta maamuzi yote ya Baraza la Uongozi la nchi hiyo, Martin Kobler, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ameelezea wasiwasi wake kufuatia kushtadi mapigano, kusini mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Fayez al Sarraj, mkuu wa Baraza la Uongozi na Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya, amechukua hatua ya kufuta maamuzi yote ya baraza hilo ikiwa ni ishara ya wazi ya namna mzozo ulivyochachamaa baina yake na wajumbe wa baraza hilo. Al Sarraj anaamini kuwa, baadhi ya wajumbe wa baraza hilo wamechukua maamuzi ya kichochezi bila ya kuwashirikisha wajumbe wote.
Vile vile anaamini kuwa Baraza la Uongozi la Libya ni kikwazo cha kufikiwa maafikiano kati ya makundi ya nchi hiyo. Fayez al Sarraj amefuta maamuzi yote ya baraza hilo katika hali ambayo tarehe 19 Januari mwaka jana 2016, ni baraza hilo ndilo lililompigia kura ya kuwa Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya.
Hata hivyo, si Fayez al Sarraj pekee anayelalamikia utendaji wa baraza hilo. Musa al-Koni, Makamu wa Rais wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya naye hivi karibuni alilikosoa baraza hilo na kuamua kujiuzulu ikiwa ni kuonesha kuchukizwa kwake na kushindwa baraza hilo kuleta utulivu nchini Libya.
Baraza la Uongozi la Libya linaundwa na watu 9 kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa mwezi Disemba 2015 huko nchini Morocco. Kwa mujibu wa makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa, serikali ya umoja wa kitaifa ilibidi iunde nchini Libya. Hata hivyo, licha ya kupita zaidi ya mwaka mmoja tangu kufikiwa makubaliano hayo, hadi hivi sasa Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ameshindwa kuunda Baraza la Mawaziri la serikali hiyo na hivyo kuifanya Libya iendelee kukosa serikali kuu.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, serikali iliyoundwa mashariki mwa Libya ambayo inaungwa mkono na Jenerali Mstaafu Khalifa Haftar, Mkuu wa Jeshi la Taifa la Libya, ina nguvu zaidi kuliko serikali ya umoja wa kitaifa ya Waziri Mkuu Fayez al Sarraj. Hivi sasa serikali hiyo ya umoja wa kitaifa imezidi kuwa dhaifu kutokana na kujiuzulu Makamu wa Rais wa serikali hiyo pamoja na hatua ya Fayez al Sarraj ya kukosoa utendaji wa Baraza la Uongozi la nchi hiyo.
Zaidi ya hayo ni kuwa, hali hiyo inaonesha kwamba, makubaliano ya mwezi Disemba 2015 yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa yanaelekea kusambaratika. Wachambuzi hao wa mambo wanasema, ishara za kukaribia kusambaratika makubaliano hayo ziko wazi. Hivi sasa Makamu wa Rais wa serikali ya umoja wa kitaifa amejiuzulu, Waziri Mkuu wa serikali hiyo analishambulia kwa maneno Baraza la Uongozi na bila ya shaka wajumbe wa baraza hilo nao hawaridhishwi na jambo hilo, hivyo kuna uwezekano hata wa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Fayez al Sarraj na kumvua uwaziri mkuu.
Huku hali ikiwa hivyo, Martin Kobler, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya, jana Jumatano tarehe 4 Januari 2017 alielezea wasiwasi wake wa kushtadi mgogoro kusini mwa Libya na kuongezeka mapigano baina ya makundi hasimu yenye silaha. Kobler ameyataka makundi yote kuvumiliana, na kuonya kuwa mizozo ndani ya Baraza la Uongozi la Libya ni ishara ya kukwama juhudi za kimataifa za kuutatua mgogoro wa nchi hiyo. Ikumbukwe kuwa, Libya haijawahi kushuhudia utulivu tangu mwaka 2011 alipopinduliwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi na tangu mwezi Agosti 2014 imekuwa ikitawaliwa na serikali mbili pamoja na mabunge mawili tofauti, huku serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa kwa usimamizi wa Umoja wa Mataifa nayo ikionekana kukwama.