Waziri wa Niger: Wapiganaji wa Boko Haram wanaojisalimisha wanazidi kuongezeka
(last modified Sat, 07 Jan 2017 03:20:23 GMT )
Jan 07, 2017 03:20 UTC
  • Waziri wa Niger: Wapiganaji wa Boko Haram wanaojisalimisha wanazidi kuongezeka

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Niger ametangaza kuwa, wanachama wengine wa kundi la kigaidi la Boko Haram wamejisalimisha kwa vyombo vya usalama vya nchi hiyo.

Mohamed Bazoum, ametangaza kuwa, karibu wanachama 20 wa kundi la kigaidi la Boko Haram walijisalimisha wiki hii kwa vikosi vya usalama vya nchi hiyo na hivyo kulifanya wimbi la wapiganaji wa kundi hilo wanaojisalimisha kuzidi kuongezeka. 

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Niger amebainisha kuwa, wanachama hao wa Boko Haram walijisalimisha katika eneo la Diffa lililoko kusuni mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Mohamed Bazoum, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Niger

Waziri huyo amesema kuwa, tangu Disemba 27 mwaka jana karibu wanachama 50 wa kundi la kigaidi la Boko Haram wamejisalimisha kwa vyombo vya usalama vya nchi hiyo na kuomba wajumuishwe katika msamaha wa umma.

Aidha amesema kuwa, wimbi la wanamgambo hao kujisalimisha linaongezeka kila siku na kwamba, vita dhidi ya kundi hilo katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo vimefikia tamati.

Nchini Chad pia maafisa wa jeshi la nchi hiyo wanasema kuwa, wanamgambo wenye mfungamano na Boko Haram wanazidi kujisalimisha kutokana na kushtadi oparesheni za kijeshi dhidi ya kundi hilo.

Nchi za Nigeria, Niger, Cameroon, Chad na Benin zimeasisi kikosi cha pamoja cha kijeshi ambacho kimepewa jukumu la  kukomesha hujuma na mashambulizi ya kundi la Boko Haram katika eneo la Ziwa Chad.  

 

Tags