Nigeria: Viongozi wa ECOWAS kutoa 'uamuzi mkubwa' juu ya Gambia
Viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) wanatazamiwa hii leo kutoa kile kilichotajwa kuwa 'uamuzi mzito' kuhusiana na mgogoro wa kisiasa unaoikabili Gambia
Garba Shehu, msemaji wa Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amesema kuwa, viongozi wa jumuiya hiyo wanatazamiwa kutoa msimamo nyeti kuhusu mzozo wa Gambia leo Jumamosi katika mkutano unaofanyika nchini Ghana. Mgogoro huo wa kisiasa uliibuka baada ya Rais Yahya Jammeh kukataa kukabidhi madaraka kwa njia ya amani kwa Adama Barrow, mfanyabiashara aliyetangazwa mshindi katika uchaguzi wa Disemba Mosi mwaka uliomalizika wa 2016.

Mkutano huu unafanyika siku chache baada ya Kamanda wa Jeshi la Gambia kutoa ujumbe akitangaza uungaji mkono kamili wa jeshi la nchi hiyo kwa Rais Yahya Jammeh.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) awali ilisema kuwa ikibidi, itatuma vikosi vya kieneo nchini Gambia, iwapo Rais Yahya Jammeh atakataa kukabidhi madaraka wakati muda wake utakapiomalizika rasmi Januari 19 mwaka huu.
Jammeh amekataa kukabidhi madaraka kwa rais mteule akidai kuwa zoezi la uchaguzi wa mwezi uliopita nchini Gambia lilitawaliwa na dosari nyingi na anataka uchaguzi wa rais ufanyike tena.
