Rais Museveni amteua mwanawe kuwa mshauri mkuu; je anamtayarisha kuja kumrithi?
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23257-rais_museveni_amteua_mwanawe_kuwa_mshauri_mkuu_je_anamtayarisha_kuja_kumrithi
Rais Yoweri Museveni wa Uganda amemteua mwanawe Meja Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kuwa mshauri mkuu wa rais katika operesheni maalumu; hatua ambayo inatajwa na baadhi ya wachambuzi wa mambo kwamba, ni ya kumuandaa mwanawe huyo aje kuchukua uongozi wa juu nchini humo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 11, 2017 03:43 UTC
  • Rais Museveni amteua mwanawe kuwa mshauri mkuu; je anamtayarisha kuja kumrithi?

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amemteua mwanawe Meja Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kuwa mshauri mkuu wa rais katika operesheni maalumu; hatua ambayo inatajwa na baadhi ya wachambuzi wa mambo kwamba, ni ya kumuandaa mwanawe huyo aje kuchukua uongozi wa juu nchini humo.

Jenerali Kainerugaba amekuwa kamanda wa kikosi maalumu cha wanajeshi (SFC) chenye jukumu la kutekeleza operesheni maalumu za kijeshi. Kikosi hicho husimamia ulinzi wa rais na kulinda maeneo muhimu ya serikali ya Uganda. Msemaji wa jeshi la Uganda, Paddy Ankunda amesema kuwa, Meja Jenerali Kainerugaba ameteuliwa kuwa mshauri wa Rais katika operesheni maalumu, lakini alipoulizwa kama hatua hiyo inalenga kumuandaa kisiasa mtoto huyo wa Museveni, Paddy Akunda alikana hilo na kueleza kuwa, ni mabadiliko ya kawaida tu.

Hatua hiyo imekosolewa vikali na wapinzani na hata mashirika ya kutetea haki za binadamu ambayo yanasema kuwa, hatua hiyo ni ya kumuandaa jenerali huyo ili aje kumrithi Rais Museveni.

Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda

Wapinzani nchini Uganda wanamtuhumu Rais Museveni kwamba, anakabidhi taratibu madaraka ya nchi kwa familia yake.

Ikumbukwe kuwa, Salim Saleh ambaye ni kaka wa Rais Museveni ni miongoni mwa washauri wa Rais huyo wa Uganda. 

Aidha mke wa Rais Museveni  Bi Janet Museveni anahudumu serikalini akiwa ni Waziri wa Elimu na Michezo.

Rais Museveni mwenye umri wa miaka 72 amekuwa madarakani nchini Uganda tangu mwaka 1986 huku wapinzani wakiendelea kuituhumu serikali yake kwamba, inakandamiza vyama vya upinzani.