Mfamle Mumbere wa Uganda kizimbani, kujua hatima yake leo
Mfalme wa Rwenzururu eneo la Rwenzori nchini Uganda, Charles Wesley Mumbere, ambaye anazuiliwa na vyombo vya usalama kwa tuhuma za uhaini anatazamiwa kujua hatima yake leo atakapofikishwa mahakamani.
Mfamle huyo anakabiliwa na mashitaka ya uhaini, mauaji, ugaidi na kuchochea machafuko yaliyotokea mjini Kasese Novemba mwaka jana, ambapo makumi ya watu wakiwemo maafisa wa polisi waliuawa.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Jinja, Eva Luswata hapo jana alisema mfamle huyo ana haki ya kisheria ya kuomba kuachiwa huru kwa dhamana.
Mmoja wa mawakili wa mfamle huyo, Evans Ochieng amesema wadhamini wa mfamle huyo watafika mahakamani leo, akiwemo Winfred Kiiza, kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Mbunge wa Busongora Kaskazini William Nzoghu, Mbuge wa Manispaa ya Kasese Centenary Franco Robert na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Rwenzururu, Constantine Bwambale.
Hapo jana mwasheria wa serikali Alex Ojok alipinga wito huo wa kupewa dhamana Mflme wa Rwenzururu, akisisitiza kuwa kuachiwa kwake huru kutatatiza uchunguzi wa polisi sambamba na kukamatwa kwa washukiwa wengine.
Makumi ya wafuasi wa Mfalme Mumbere wanaounga mkono mfumo wa kifalme nchini Uganda pamoja na maafisa 16 wa polisi waliuawa katika mapigano hayo yaliyotokea mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka jana, katika mji wa Kasese mpakani mwa Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Tayari kundi la wabunge wa upinzani nchini Uganda limetuma ombi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, likiitaka ianzishe uchunguzi juu ya mauaji hayo yanayodaiwa kufanywa na maafisa usalama katika mji wa Kasese, jimbo la Rwenzori.