Gaddafi: Baba yangu hakumteka nyara Imam Musa Sadr
-
Hannibal Muammar Gaddafi, mwana wa kiume wa kiongozi wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi
Hannibal Muammar Gaddafi, mwana wa kiume wa kiongozi wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi amsema kuwa, Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo ndiye aliyemteka nyara Imam Musa Sadr
Shirika la habari la wanafunzi wa vyuo vikuu wa Iran ISNA limemnukuu Hannibal Muammar Gaddafi akidai kuwa, Abdessalam Jalloud, Waziri Mkuu wa zamani wa Libya ambaye alikuwa kiongozi nambari mbili wa nchi hiyo wakati wa utawala wa Mummar Gaddafi ndiye aliyemteka nyara Imam Musa Sadr na msafara wake na kwamba baba yake, yaani Kanali Muamad Gaddafi hakuhusika na jambo hilo.
Hannibal Gaddafi alitiwa mbaroni nchini Lebanon mwezi Disemba 2015. Hii ni mara ya kwanza kwa Hannibal Gaddafi kukiri kuwa Imam Musa Sadr alitekwa nyara akiwa nchini Libya.
Mwana huyo wa kiongozi wa zamani wa Libya pia amemtuhumu Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo kwamba ndiye aliyesababisha kuharibika uhusiano wa nchi yake na Misri katika kipindi cha Rais Anwar Sadat, kama ambavyo pia amemtuhumu kuchochea vita baina ya Chad na Libya.
Suala la kutoweka Imam Musa Sadr na wenzake nchini Libya limekuwa ni kitendawili kikubwa kwa miaka 40 sasa huko nchini Lebanon.
Mwaka 1978, Imam Musa Sadr, mwasisi wa harakati ya Amal ya Lebanon alikwenda nchini Libya kwa mwaliko rasmi wa Kanali Muammar Gaddafi, lakini hadi hivi sasa hatima yake na wenzake wawili haijulikani.