Sheikh Zakzaky atoa ujumbe akiwa katika jela ya serikali ya Nigeria
Duru za habari nchini Nigeria zimeripoti kuwa kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ametoa ujumbe akiwa katika korokoro ya serikali ya nchi hiyo.
Duru za kuaminika zinasema kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye anashikiliwa katika jela ya Nigeria ametoa ujumbe akisema hana wasiwasi kuhusu kuendelea kushikiliwa jela au kuachiwa huru, kwa sababu Mwenyezi Mungu Muweza huwatunuku kheri waja wake popote pale wanapokuwa.
Wakati huo huo msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Shekih Ibrahim Mussa ameitahadharisha serikali ya nchi hiyo kutokana na kupuuza amri ya mahakama iliyoiamuru kumwachia huru Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Ripoti zinasema kuwa serikali ya Nigeria haijachukua hatua yoyote ya kumwachia huru au kubadilisha mwenendo wake kuhusu Sheikh Ibrahim Zakzaky na kwamba jeshi la Nigeria linakwamisha uamuzi huo.
Muhula wa mwisho ulioainishwa na Mahakama Kuu ya Nigeria kwa ajili ya kuachiwa huru kiongozi wa Waislamu wa Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky unamalizika leo Jumatatu.
Mapema mwezi Disemba mwaka uliopita Jaji Gabriel Kolawole wa Mahakama Kuu ya Nigeria aliiamuru serikali na Nigeria kumwachilia huru bila ya masharti yoyote Sheikh Zakzaky na mke wake katika kipindi cha siku 45 zijazo.
Hukumu ya mahakama hiyo ilisema kuwa, kuendelea kushikiliwa Sheikh Zakzaky gerezani bila ya kufikishwa mahakamani ni kukiuka haki zake zinazosisitizwa katika katiba ya Nigeria na kwamba madai ya serikali kwamba inamshikilia Sheikh Zakzaky gerezani kwa shabaha ya kulinda usalama wake na mkewe, hayawezi kukubalika.
Disemba 13 mwaka 2015 jeshi la Nigeria lilifanya hujuma dhidi ya Husseiniyah ya Baqiyatullah na makazi ya Sheikh Zakzaky mjini Zaria. Waislamu zaidi ya elfu moja waliuawa kwa umati mamia ya wengine akiwa Sheikh Zakzaky pamoja na mkewe walitiwa nguvuni.