Waislamu wa Nigeria wanasubiri kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky
Sambamba na kukaribia wakati wa kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, msemaji wa harakati hiyo amewatahadharisha viongozi wa nchi hiyo na kuwataka wamuachilie huru haraka iwezekanavyo mwanaharakati huyo wa Kiislamu.
Ibrahim Mussa, Msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ametoa taarifa maalumu ambapo mbali na kutahadharisha kuhusiana na kupuuzwa amri ya mahakama ya nchi hiyo kuhusiana na kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky amesisitiza kuwa, njama za viongozi wa serikali ya Abuja za kuchafua sura ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria hazitazaa matunda.
Ibrahim Mussa ameeleza kuwa, nyaraka zilizofichuliwa na duru za kuaminika na ambazo ziko karibu na mashirika ya kijasusi ya nchi hiyo zinaonesha kuwa, baadhi ya mamluki wa ndani na wa nje wanafanya njama za kukiuka amri ya mahakama inayotaka kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky.
Wakati huo huo, Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye anashikiliwa katika jela ya Nigeria ametoa ujumbe akisema hana wasiwasi kuhusu kuendelea kushikiliwa jela au kuachiwa huru, kwa sababu Mwenyezi Mungu Muweza huwatunuku kheri waja wake popote pale walipo.
Disemba mwaka 2015 jeshi la Nigeria lilifanya hujuma dhidi ya Husseiniyah ya Baqiyatullah na makazi ya Sheikh Zakzaky mjini Zaria. Waislamu zaidi ya elfu moja waliuawa kwa umati huku Sheikh Zakzaky pamoja na mkewe wakitiwa nguvuni. Kila mara kumekuwa kukiripotiwa habari za kuzorota afya ya mwanaharakati huyo huko anakoshikiliwa.
Tangu kiongozi huyo wa Waislamu atiwe mbaroni kumekuweko mashinikizo ya kila upande ya kutaka kuachiliwa huru mwanaharakati huyo. Aidha tangu lilipotokea tukio la kuuawa mamia ya Waislamu wa Nigeria, Waislamu wa nchi hiyo wamekuwa wakiandamwa na mashinikizo kutoka kwa vikosi vya usalama vya nchi hiyo.
Akthari ya Waislamu wa Nigeria wamekuwa wakifanya mikusanyiko na maandamano mara kwa mara wakitaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky. Licha ya afya ya Sheikh Zakzaky kuwa mbaya, lakini viongozi wa serikali ya Nigeria wameendelea kumshikilia korokoroni mwanaharakati huyo. Mashinikizo ya Waislamu dhidi ya serikali nchini Nigeria yameshadidi kiasi cha kuvifanya vikosi vya usalama kuamiliana vibaya mno na waandamanaji huku serikali ikipiga marufuku mikusanyiko ya aina yoyote ile.
Pamoja na hayo yote, katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, takwa kuu la Waislamu wa Nigeria limekuwa ni kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky. Kufuatia mashinikizo hayo ya Waislamu, Mahakama Kuu ya Nigeria ilithibitisha kutokuwa na hatia Sheikh Zakzaky na ikaiamuru serikali na Nigeria kumuachilia huru bila ya masharti yoyote Sheikh Zakzaky pamoja na mke wake katika kipindi cha siku 45. Kwa mujibu wa amri ya mahakama, katika siku hizi hizi Sheikh Zakzaky anapaswa kukabidhiwa kwa maafisa wa polisi ambao pia wanapaswa kumuachilia huru yeye pamoja na mkewe katika kipindi cha masaa 24.
Hata hivyo licha ya amri hiyo ya mahakama hadi leo hakushuhudiwi hatua au ishara ya kubadilika mwenendo wa vyombo vya usalama kwa ajili ya kumuachilia huru Sheikh Zakzaky. Ni kwa kuzingatia uhalisia huo ndio maana dhana ya kwamba, kuna njama za kutotekelezwa amri ya mahakama inapata nguvu. Hivi karibuni baadhi ya duru ziliripoti kwamba, Sheikh Zakzaky na mkewe wamehamishiwa mahala kusikojulikana.
Hivi sasa Waislamu wa Nigeria wanahesabu saa wakisubiri kuachiliwa huru kiongozi wao huyo na hatua yoyote ile ya kuchelewesha kutekeleza hukumu hiyo ya mahakama inahesabiwa na Waislamu hao kuwa ni mstari mwekundu. Hapana shaka kuwa, kucheleweshwa kutekelezwa amri hiyo ya mahakama hasa kwa kuzingatia mazingira ya kisiasa na kiuchumi inayokabiliwa nayo Nigeria kwa sasa, kunaweza kuwa na taathira hasi na mbaya katika umoja wa wananchi wa nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika na hivyo kuweka vingiti katika njia ya utatuzi wa matatizo mengine ya nchi hiyo.