Wahajiri 219 wamezama katika Bahari ya Mediterranea
(last modified Wed, 18 Jan 2017 04:09:27 GMT )
Jan 18, 2017 04:09 UTC
  • Wahajiri 219 wamezama katika Bahari ya Mediterranea

Wahajiri na wakimbizi wapatao 219 wamezama katika Bahari ya Mediterranea katika wiki mbili za kwanza za mwaka 2017 hii ikiwa ni mara mbili zaidi ya kipindi sawa na hiki mwaka jana.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), katika tukio moja pekee siku chache zilizopita watu 180 walipoteza maisha wakati boti yao ilipozama katika pwani ya Libya. Msemaji wa IOM, Joel Millman akizungumza mjini Geneva amesema kwa kuzingatia idadi hiyo, watu waliopoteza maisha mwaka huu wakijaribu kuingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranea ni 219. Amesema maafisa wa IOM pia wanachunguza ripoti kuwa wahamiaji wengine 25 wamepoteza maisha baada ya boti yao kuzama baina ya Morocco na Uhispania hivi karibuni.

Wahajiri wakijaribu kuingia Ulaya

Shirika la Kimataifa la Uhajiri limetangaza wakimbizi na wahajiri zaidi ya 5,000 walipoteza maisha mwaka jana wa 2016 wakijaribu kuingia barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranea.

Mwezi Novemba mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilianzisha uchunguzi juu ya biashara haramu ya kuwasafirisha wahajiri wa Kiafrika wanaopelekwa barani Ulaya kupitia usafiri hatari wa baharini.

Aghalabu ya wahajiri wanaopoteza maisha wakijaribu kutumia njia bahari kuingia Ulaya ni kutoka nchi za Mashariki ya Kati na bara Afrika.

 

Tags