Libya yawaachia huru wahamiaji 82 waliokuwa wametekwa na wahalifu
Mamlaka za Libya zimetangaza habari ya kuwaachilia huru wahamiaji 82 waliokuwa wakishikiliwa mateka na kundi la wahalifu likidai kikomboleo.
Polisi ya Wilaya ya Jufra imesema katika taarifa ya jana Jumanne kwamba, wahamiaji hao waliteswa na kubakwa ili kuzilazimisha familia zao kulipa maelfu ya dola ili waachiwe huru.
Wanachama wanne wa kundi hilo la uhalifu walikamatwa katika mji wa kati wa Zillah, yapata kilomita 750 kusini mashariki mwa mji mkuu Tripoli, ambapo wahamiaji hao walikuwa wamezuiliwa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Libya imesema.
Mmoja wa washukiwa waliokamatwa alikiri kwamba wahamiaji 10 waliteswa hadi kufa wakiwa mateka, na kwamba walidai kikomboleo cha hadi dola 10,000 za Marekani kwa kila mateka.
Mwezi uliopita, Polisi wa Wilaya ya Jufra waliripoti kukamatwa kwa kundi la wafanya magendo wa wahamiaji huko Zillah, waliotuhumiwa kuwaua wahajiri na kuzika miili yao jangwani, mbali na utekaji nyara, kuweka na njaa, ubakaji na kuwauza wahamiaji hao kwa bidhaa.
Kutokana na hali ya ukosefu wa usalama na machafuko nchini Libya tangu kutumuliwa madarakani na kuuawa Muammar Gaddafi mwaka 2011, wahamiaji wengi, hasa kutoka Afrika, huchagua kuvuka Bahari ya Mediterania kuelekea Ulaya kupitia Libya.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), wahamiaji karibu 5,000 wamekamatwa na kurejeshwa Libya, huku 82 wakiripotiwa kufa maji, na wengine 58 kutoweka katika maji ya Mediterania.