Bunge la Gambia lamuongezea Jammeh miezi 3, Nigeria yatuma manowari
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23827-bunge_la_gambia_lamuongezea_jammeh_miezi_3_nigeria_yatuma_manowari
Bunge la Taifa la Gambia limepasisha azimio la kumruhusu Rais Yahya Jammeh wa nchi hiyo asalie madarakani kwa miezi mitatu zaidi katika hali ambayo muda wake wa kuhudumu unaelekea kumalizika.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 18, 2017 16:40 UTC
  • Bunge la Gambia lamuongezea Jammeh miezi 3, Nigeria yatuma manowari

Bunge la Taifa la Gambia limepasisha azimio la kumruhusu Rais Yahya Jammeh wa nchi hiyo asalie madarakani kwa miezi mitatu zaidi katika hali ambayo muda wake wa kuhudumu unaelekea kumalizika.

Wadadisi wa mambo wanasema hatua hiyo ya Bunge la Taifa la Gambia inapania kuzuia sherehe za kuapishwa Rais-mteule wa nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika, Adama Barrow, ambaye kwa sasa yuko nchini Senegal.

Hayo yamearifiwa katika hali ambayo, vyombo vya habari vya Nigeria vimesema moja ya meli za kivita za nchi hiyo imeng'oa nanga kuelekea Gambia, katika kile kinachoonekana ni kuviweka katika hali ya tahadhari vikosi vya kieneo.

Captain Dahun Jahun, msemaji wa Jeshi la Majini la Nigeria amesema kuwa, jeshi la nchi hiyo litachangia askari 200 ambao wamewekwa katika hali ya tahadhari tayari kutumwa nchini Gambia.

Adama Barrow, Rais mteule wa Gambia

Aidha majeshi ya Ghana na Senegal yamesema yatatuma wanajeshi wao nchini Gambia, kwa mujibu wa ilivyotishia Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS, iwapo Jammeh ataendelea kung'ang'ania madaraka muda wake ukimalizika kesho Alkhamisi Januari 19.

Jana Rais Yahya Jammeh wa Gambia alitangaza hali ya hatari nchini humo kwa siku 90 akiashiria kuingiliwa na nchi ajinabi uchaguzi wa rais wa nchi hiyo uliofanyika mwezi Disemba mwaka jana. Halifa Sallah, msemaji wa Adama Barrow amesema kuwa, ikibidi, Rais mteule wa Gambia ataapishwa kesho katika ubalozi wa Gambia nchini Senegal.

Wakati huo huo, mamia ya wananchi wa Gambia wameanza kuondoka nchini humo wakikimbilia usalama wao katika nchi jirani. Thomas Cook, afisa wa masuala ya utalii raia wa Uingereza amesema wameanza kuondoa watalii1000 hii leo huku wengine 2,500 wakitazamiwa kuondolea nchini humo hivi karibuni.