Taasisi za kimataifa zatangaza kuwa tayari kuwasaidia wakimbizi wa Gambia
Mashirika ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu yameelekeza nguvu zao kwenye kuwasaidia wakimbizi wa Gambia ambao katika wiki za hivi karibuni wamekimbilia nchi jirani kuokoa maisha yao.
Babar Baloch, msemaji wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amesema, mashirika mbalimbali ya misaada ya kibinadamu ukiwemo Umoja wa Mataifa yametangaza kuwa kwao tayari kuwasaidia kwa hali na mali wakimbizi wa Gambia. Serikali ya Senegal imetangaza kuwa, karibu raia 45 elfu wa Gambia wameingia nchini humo siku za hivi karibuni kutokana na hali mbaya ya kisiasa na uwezekano wa kutokea vita nchini Gambia.
Idadi wa wakimbizi wa Gambia iliongezeka sana baada ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS kutangaza kuwa itatuma jeshi la nchi kadhaa huko Gambia kwa lengo la kumuondoa madarakani kwa nguvu Yahya Jammeh na kurejesha utawala wa katiba nchini humo.
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema kuwa, zaidi ya asilimia 75 ya raia wa Gambia waliokimbilia nchi jirani ya Senegal ni wanawake na watoto wadogo. Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limetangaza kuwa, fikra za walio wengi zimeelekeza macho na masikio yake kwenye mgogoro wa kisiasa wa Gambia wakati ambapo maelfu ya wanawake na watoto wadogo wamelazimika kukimbilia Senegal kwa ajili ya kulinda usalama wao.
Baada ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS kutishia kutuma wanajeshi wake nchini Gambia, serikali ya Senegal iliingiza wanajeshi wake ndani ya ardhi ya nchi hiyio kama ambavyo pia ilitumia ubalozi wa Gambia mjini Dakar, Senegal kuwa eneo la kumwapisha Adama Barrow kuwa Rais mpya wa Gambia.