Wanasheria wataka Sheikh Zakzaky aachiwe huru
Wanasheria na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Nigeria wametoa wito wa kufikishwa mahakamani viongozi wa jimbo la Kaduna huko kaskazini mwa nchi hiyo kutokana na kukwamisha zoezi la kuachiwa huru kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Femi Falana ambaye ni mwanasheria na mtetetezi wa haki za bindamu nchini Nigeria ametoa taarifa akisisitiza udharura wa kufikishwa mahakamani maafisa usalama walioshambulia makazi ya Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini humo, Sheikh Ibrahim Zakzaky na kusema, viongozi wa jimbo la Kaduna wanapaswa kuhukumiwa kutokana na kulisaidia jeshi la Nigeria katika uhalifu huo na kutotoa kibali cha kufikishwa mahakamami wale walioshambulia nyumba ya Sheikh Zakzaky na Waislamu wa mji wa Zaria.
Taarifa hiyo imetolewa huku Waislamu wa madhehebu ya Shia wakiendela kufanya maandamano katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo wakipinga marufuku ya mikusanyiko na kufuatilia haki zao za kisheria.
Disemba mwaka juzi, jeshi la Nigeria lilishambulia msikiti na kituo cha kidini cha Baqiyatullah katika mji Zaria na kumtia mbaroni Sheikh Ibrahim Zakzaky, mkewe na makumi ya wanachama wa Harakati ya Kiislamu baada ya kuwauwa shahidi mamia ya wafuasi wa harakati hiyo waliokuwa kwenye shughuli ya kidini.