Barrow: Askari wa ECOWAS kuendelea kusimamia amani Gambia
Rais mpya wa Gambia, Adama Barrow amewataka askari wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS, kusalia nchini humo kwa lengo la kusimamia usalama na amani.
Ahmed Fati, wakili, mshauri na msemaji wa rais huyo amesema kuwa, licha ya Yahya Jammeh kuondoka madarakani, lakini hadi sasa bado kuna kundi kubwa la wafuasi wa rais huyo wa zamani wa Gambia. Kwa mujibu wa Fati kuwepo askari wa ECOWAS, ni suala muhimu kwa serikali mpya ya Rais Adama Barrow kwa ajili ya kusimamia amani na utulivu nchini humo.
Sambamba na kuonyesha wasi wasi wake juu ya hali ya mambo nchini humo, amewataka raia wa Gambia kushikamana na kuwa kitu kimoja katika kipindi hiki muhimu cha kujiri mabadiliko ya kisiasa ndani ya taifa hilo la magharibi mwa Afrika.