Fahamu maslahi ya Senegal katika kufanikisha mabadiliko ya uongozi nchini Gambia
Sambamba na Senegal kutatua mgogoro wa kisiasa nchini Gambia na kufanikisha mabadiliko ya uongozi nchini humo, lakini inaonekana kuwa katika kufanya hivyo serikali ya Dakar pia ilikuwa ikizingatia maslahi yake katika uwanja huo.
Senegala ni moja ya nchi ambazo zimehusika pakubwa katika utatuzi wa mgogoro wa kisiasa wa Gambia, huku ikiandaa kikosi cha jeshi pamoja na Nigeria kwa ajili ya kumuondoa kwa nguvu madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Yahya Jammeh. Hatua hiyo ilichukuliwa na serikali ya Dakar, baada ya Jammeh kusisitizia kusalia madarakani sanjari na kupinga matokeo ya uchaguzi uliopita na ambao ulimpa ushindi hasimu wake Adama Barrow.
Hata hivyo upatanishi uliofanywa na nchi za eneo la magharibi mwa Afrika na kadhalika tishio la shambulizi la kijeshi la nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS), lilimfanya rais huyo wa zamani aliyeitawala Gambia kwa miaka 22, kuondoka madarakani na kukimbilia uhamishoni. Hata hivyo baada ya yote hayo, kunaibuka swali hili kwamba, je, Senegal imefaidika na nini katika juhudi zote hizo za mabadiliko ya kiutawala nchini Gambia? Ni suala lililo wazi kwamba, Gambia ni nchi iliyozungukwa na Senegal. Katika kipindi cha uongozi wa Jammeh, nchi hiyo iligeuka na kuwa ngome ya eneo linalopigania kujitenga la Casamance katika ardhi ya Senegal. Kwa mtazamo wa Wasenegal, Jammeh alitumia suala la kujitenga eneo la Casamance kama msingi mkuu wa kuweza kuishinikiza serikali ya Dakar.
Yoro Dia, mtaalamu wa masuala ya kisiasa ya Senegal amezungumzia juhudi za Rais Macky Sall wa Senegal za kuhitimisha kadhia ya Yahya Jammeh kwa kusema, wakati ambao rais huyo wa zamani wa Gambia alipokuwa akizungumzia amani, kwa upande mwingine alikuwa akiunga mkono harakati za kutaka kujitenga eneo la Casamance. Kwa upande mwingine serikali ya Senegal ina matumaini kwamba kuingia madarakani Adama Barrow kutaweza kuzuia magendo ya miti ya eneo la Casamance kwenda China, kama ambavyo pia itaweza kuhitimisha magendo ya madawa ya kulevya. Hayo yanajiri katika hali ambayo baada ya kukubali kuachia ngazi na kukabidhi madaraka kwa njia ya amani, rais huyo wa zamani wa Gambia, ameenda uhamishoni nchini Equatorial Guinea.
Kwa mujibu wa Marcel Alain de Souza, Msemaji wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS, Jammeh alielekea nchini Equatorial Guinea muda mfupi baada ya kuwasili katika mji mkuu wa Guinea, Conackry hapo juzi Jumamosi ambapo aliandamana na Rais Alpha Conde wa Guinea Conackry. Hata hivyo licha ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS kutangaza kuwa, Jammeh hatakabiliwa na hatua zozote za kisheria, au kupokonywa mali zake kama ambavyo jumuiya hiyo haitaruhusu mtu au taasisi yeyote ikiuke haki, hadhi na usalama wake pamoja na familia yake, lakini rais mpya wa Gambia Adama Barrow amesema serikali yake itaunda Tume ya Ukweli na Maridhiano itakayokuwa na jukumu la kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki za binadamu ya serikali ya Jammeh katika utawala wake wa miaka 22.