Kuweko maridhiano ya kitaifa Burundi; lengo la mkutano wa wapinzani nchini Ubegiji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24203-kuweko_maridhiano_ya_kitaifa_burundi_lengo_la_mkutano_wa_wapinzani_nchini_ubegiji
Sambamba na kuendelea mgogoro wa kisiasa nchini Burundi, wapinzani wa serikali ya Bujumbura wamefanya kikao nchini Ubegiji kilichokuwa na lengo la kuandaa mikakati ya pamoja dhidi ya serikali ya Bujumbura.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 25, 2017 02:57 UTC
  • Kuweko maridhiano ya kitaifa Burundi; lengo la mkutano wa wapinzani nchini Ubegiji

Sambamba na kuendelea mgogoro wa kisiasa nchini Burundi, wapinzani wa serikali ya Bujumbura wamefanya kikao nchini Ubegiji kilichokuwa na lengo la kuandaa mikakati ya pamoja dhidi ya serikali ya Bujumbura.

Wawakilishi wa kisiasa wa upinzani, jumuiya za kiraia na Waburundi wanaoishi nje ya nchi ambao wanapinga hatua ya Rais Nkurunziza ya kuchukua madaraka ya nchi kwa mara ya tatu mfululizo wameshiriki katika mkutano huo nchini Ubelgiji. Duru za karibu na mkutano huo zinasema lengo lake kuu ni kuandaa mikakakti ya pamoja kwa ajili ya kuchukua maamuzi ya kurejesha demokrasia na utawala wa katiba nchini Burundi.

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi

Shakhsia 34 wa kisiasa na wawakilishi wa jumuiya za kiraia ambao wamekimbia machafuko ya Burundi walishiriki katika mkutano huo wa Ubegiji.  Washiriki wa mkutano huo wamefikia makubaliano ya kuchukua hatua za lazima za kupambana kwa amani kwa ajili ya kuleta demokrasia katika nchi hiyo na kuundwa kamati ya maridhiano ya kitaifa na upatanishi. Burundi ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa tangu mwaka 2015, kufuatia hatua ya Nkurunziza kutangaza nia yake ya kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tatu. Wapinzani kwa upande wao waliitaja  hatua hiyo ya Nkurunziza kuwa ni kinyume na katiba na kumtuhumu kuwa amepuuza makubaliano ya amani ya Burundi yaliyohitimisha vita vya ndani nchini humo. 

​Tangu uchaguzi huo uliolalamikiwa kieneo na kimataifa ufanyike na Nkurunziza kuchaguliwa kuongoza tena Burundi, nchi hiyo imekuwa ikishuhudia wimbi la machafuko, mauaji na kamatakamata dhidi ya wapinzani. Ripoti za mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu zinaonyesha kuwa, wapinzani nchini Burundi wamekuwa wakilengwa na vitendo vya utumiaji mabavu. Machafuko nchini Burundi yamepekea mamia ya raia wa Burundi kuuawa huku maelfu ya wengine wakilazimika kuwa wakimbizi katika nchi jirani. Licha ya ripoti nyingi kuonyesha kwamba, kumekuweko na vitendo vya ukandamizaji dhidi ya wapinzani nchini Burundi, lakini Rais Nkurunziza na serikali yake wanapinga hilo na badala yake wanasisitiza kwamba, hali ya mambo nchini humo ni nzuri. 

Wakimbizi wa Burundi

Nkurunziza anaamini kuwa, nchi zingine zikiwemo Rwanda na Ubelgiji zimekuwa zikiwasaidia wapinzani ili waiangushe serikali yake. Burundi ambayo ni koloni la zamani la Ubelgiji inaamini kuwa, mazingira ya sasa yanayotawaka nchini humo ni natija ya uingiliaji wa Brussels katika masuala ya ndani ya nchi hiyo ndogo ya Kiafrika.

Hii ni katika hali ambayo, wapinzani nchini Burundi wanasema, anga iliyojitokeza hivi sasa nchini humo ni matokeo ya kukosekana uhuru wa kisiasa na kijamii na kutoheshimiwa demokrasia sambamba na kukiukwa katiba ya nchi kulikofanywa na Rais Nkurunziza.

Benjamin Mkapa mpatanishi wa EAC katika mgogoro wa Burundi akiwa na Rais Nkurunziza

Hata kama hadi sasa jumbe mbalimbali zikiwa katika muundo wa upatanishi zimefanya safari nchini Burundi na hata kufanya mazungumzo, lakini juhudi hizo hazijaweza kupelekea kupatikana maridhiano ya kitaifa katika nchi hiyo. Serikali ya Rais Nkurunziza ikiwa na nia ya kutuliza hali ya mambo, imeachilia huru baadhi ya wafungwa wa kisiasa.

Hivi sasa inaonekana kuwa, wapinzani nje ya Burundi wanafanya juhudi za kutatuliwa mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo sambamba na kupatikana maridhiano ya kitaifa. Hii ni katika hali ambayo, nchi za kieneo na asasi za kimataifa nazo zinataka kuhitimishwa mgogoro wa kisiasa wa Burundi na kurejeshwa amani na uthabiti wa nchi hiyo kwa kushirikishwa makundi na mirengo yote ya kisiasa. Sasa tusubiri na kuona chama tawala na Rais Nkurunziza kitasaidia kwa kiwango gani juhudi za kurejesha demokrasia na kuboresha hali ya kisiasa na kijamii nchini humo.