Morocco yatishia kuvunja uhusiano wa kiuchumi na EU
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24789-morocco_yatishia_kuvunja_uhusiano_wa_kiuchumi_na_eu
Serikali ya Morocco imetishia kuvunja uhusiano wake wa kiuchumi na Umoja wa Ulaya (EU).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 07, 2017 00:31 UTC
  • Morocco yatishia kuvunja uhusiano wa kiuchumi na EU

Serikali ya Morocco imetishia kuvunja uhusiano wake wa kiuchumi na Umoja wa Ulaya (EU).

Kwa mujibu wa gazeti la Kifaransa la La Figaro, serikali ya Morocco ilitoa taarifa jana Jumatatu na kutangaza kuwa endapo Umoja wa Ulaya hautatekeleza mkataba wa kibiashara wa bidhaa za kilimo uliosaini na Morocco, nchi hiyo itahatimisha ushirikiano wake wa kiuchumi na umoja huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na serikali ya Rabat, mikataba ya kibiashara ya EU na nchi hiyo imewezesha kupatikana maelfu ya ajira katika sekta ya kilimo; na kubaki bila kazi watu waliopatiwa ajira hizo kutazusha wimbi jipya la uhajiri kuelekea nchi za Ulaya.

Mnamo mwezi uliopita wa Januari, Mahakama ya Uadilifu ya Umoja wa Ulaya (CJUE), ilitoa uamuzi wa kubatilisha mikataba ya biashara katika sekta za bidhaa za kilimo na uvuvi baina ya umoja huo na Morocco katika eneo la Sahara Magharibi ambalo limekuwa likizozaniwa kwa miaka kadhaa sasa kati ya serikali ya Morocco na harakati ya Polisario inayopigania uhuru na kujitawala eneo hilo.

Wapiganaji wa Polisario

Harakati hiyo ya ukombozi wa Sahara  Magharibi iliuelezea uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Uadilifu ya Ulaya kuwa ni ushindi kwake.

Makubaliano ya usitishaji ya mwaka 1991 yaliyofikiwa kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa yalihatimisha miaka 16 ya vita na mapigano kati ya Morocco na harakati ya Polisario inayoungwa mkono na Algeria.

Morocco inadai kuwa Sahara Magharibi ni sehemu isiyotenganishika na ardhi ya nchi hiyo…/