Mutharika: Mazungumzo mapya kuhusu mzozo wa mpaka wa Tanzania/Malawi kuanza
Rais Peter Mutharika wa Malawi amesema duru mpya ya mazungumzo ya kujaribu kuupatia ufumbuzi mzozo wa mpaka wa nchi hiyo na jirani yake, Tanzania itaanza karibuni hivi.
Rais Mutharika ameyasema hayo leo Jumanne baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mashauri ya Kigeni na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Augustine Mahiga mjini Lilongwe na kuongeza kuwa, mazungumzo hayo ambayo yalikwama mwaka 2012, yataongozwa na Rais wa zamani wa Msumbiji, Joaquim Chissano.
Amesisitiza kuwa, mazungumzo hayo yatafanyika kwa shabaha ya kufikia makubaliano ya mantiki kuhusu mvutano huo, unaohusu mpaka wa Tanzania na Malawi katika eneo la Ziwa Nyasa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mashauri ya Kigeni na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Augustine Mahiga amesema kuwa, mvutano huo unatokana na kurithiwa ramani mbili tofauti zilizoachwa na Waingereza na Wajerumani akisisitiza kuwa kuna haja ya ramani sahihi kutathminiwa na kuangaliwa kwa makini ili kuumaliza mzozo huo.
Mwishoni mwa mwaka uliomalizika 2016, mzozo wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi uliowahi kuzuka pia huko nyuma, uliibuka tena baada ya Tanzania kutoa ramani mpya, inaonyesha kuwa inamiliki nusu ya Ziwa linalozozaniwa la Malawi au Nyasa,huku Malawi ikishikilia kuwa ramani hiyo si sahihi. Malawi iliutaka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika pamoja na jumuiya na asasi zingine za kimataifa kuingilia kati suala hilo.

Mzozo baina ya nchi mbili hizo uliibuka mwaka 2011 wakati Malawi ilipoanza shughuli za kutafuta mafuta kwenye ziwa hilo. Aidha mapema miaka ya sitini, Malawi ilidai umiliki wa ziwa hilo kwa mujibu wa Makubaliano ya Heligoland ya mwaka 1890 kati ya Uingereza na Ujerumani, ambayo yalisema kuwa mpaka kati ya nchi hizo uko upande wa Tanzania.