Feb 09, 2017 07:23 UTC
  • Barrow: Vikosi vya kieneo kusalia Gambia kwa miezi mitatu zaidi

Vikosi vya kieneo vya mgharibi mwa Afrika vilivyotumwa nchini Gambia kuhakikisha usalama katika mchakato wa kushika madaraka serikali mpya ya nchi hiyo, vitasalia nchini humo kwa muda wa miezi mitatu zaidi.

Ofisi ya Rais Adama Barrow wa Gambia  imetangaza kuwa, vikosi hivyo vya kieneo vya ECOMIG vilivyotumwa nchini humo na Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS mwishoni mwa mwezi uliopita wa Januari vimeongezewa muda wa kuhudumu wa miezi mitatu.

Taarifa hiyo ya Ofisi ya Rais imeongeza kuwa, muda wa kuhudumu nchini humo vikosi hivyo vyenye askari wapatao 7000 wa kieneo huenda utaangaliwa upya baada ya miezi mitatu iwapo hilo litahitajika.  

Adama Barrow, Rais wa Gambia

Mara baada ya kurejea nchini akitokea nchi jirani ya Senegal, Barrow aliomba vikosi vya askari wa kieneo visalie nchini humo kwa miezi sita zaidi, hadi mambo yatakapotengamaa.

Barrow alirejea Gambia Januari 26 akitokea nchi jirani ya Senegal, alikokimbilia akihofia usalama wake tangu Januari 15, baada ya mtangulizi wake kung'ang'ania madaraka.

Baada ya kuchachamaa kwa muda na kukataa kukabidhi hatamu za uongozi wa nchi, aliyekuwa rais wa Gambia Yahya Jammeh hatimaye alikubali matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika Disemba Mosi mwaka jana na kungátuka madarakani kufuatia mashinikizo ya kieneo na kimataifa.

Aliyekuwa rais wa Gambia, Yayha Jammeh akiabiri ndege kuelekea Equatorial Guinea

Jammeh, ambaye aliitawala Gambia kwa muda wa miaka 22 aliondoka nchini humo na sasa yuko uhamishoni nchini Equatorial Guinea.

Tags