Mieleka yashuhudiwa tena bungeni nchini Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24947-mieleka_yashuhudiwa_tena_bungeni_nchini_afrika_kusini
Kwa mara nyingine tena Bunge la Afrika Kusini jana Alkhamisi lililegeuzwa na kuwa ukumbi wa masumbwi, mieleka na malumbano kufuatia hatua ya wabunge wa upinzani kuzusha fujo kwa lengo la kuzuia hotuba ya Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo kwa taifa.
(last modified 2026-03-17T08:06:21+00:00 )
Feb 10, 2017 08:02 UTC
  • Mieleka yashuhudiwa tena bungeni nchini Afrika Kusini

Kwa mara nyingine tena Bunge la Afrika Kusini jana Alkhamisi lililegeuzwa na kuwa ukumbi wa masumbwi, mieleka na malumbano kufuatia hatua ya wabunge wa upinzani kuzusha fujo kwa lengo la kuzuia hotuba ya Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo kwa taifa.

Maafisa wa usalama bungeni waliwatoa nje kwa nguvu wabunge wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters EFF kinachoongozwa na Julius Malema, kinara wa upinzani na mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Jacob Zuma, kufuatia agizo la Spika wa Bunge. 

Wabunge wa chama kikuu cha upinzani walikhiari kutoka kwa amani nje ya bunge wakiongozwa na kiongozi rasmi wa shughuli za upinzani bungeni, Mmusi Maimane.

Nje ya majengo ya Bunge, polisi walilazimika kufyatua mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya wafuasi wa chama cha EFF na wale wa chama tawala African National Congress ANC waliokuwa wakilumbana. 

Wabunge wa upinzani wakitolewa kwa nguvu bungeni jana

Kabla ya hapo, Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo alitoa agizo kuwa majengo ya bunge yazingirwe na wanajeshi zaidi ya 4000 wakishirikiana na maafisa wa polisi ili kutoa ulinzi wakati atakapokuwa akilihutubia taifa. Hata hivyo vyama vya upinzani vikiongozwa na EFF vilikosoa vikali agizo hilo na kulitaja kama kutangazwa vita.

Hii sio mara ya kwanza kwa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters kuzua tafrani bungeni na hatimaye kurushwa nje ya bunge. Mwezi Mei mwaka jana baada ya fujo kama za jana kushuhudiwa bungeni, Malema aliwaambia waandishi wa habari kuwa: "Sisi hatuogopi jeshi wala vita, tutapigana na ikibidi tutabeba silaha ili kuiangusha serikali fisadi iliyoko mamlakani."