UN yataka suala la wakimbizi Libya lishughulikiwe ipasavyo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25005-un_yataka_suala_la_wakimbizi_libya_lishughulikiwe_ipasavyo
Maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa wametaka kuchukuliwe hatua za kivitendo za kufuatilia hali ya wakimbizi wa nchini Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 11, 2017 13:08 UTC
  • UN yataka suala la wakimbizi Libya lishughulikiwe ipasavyo

Maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa wametaka kuchukuliwe hatua za kivitendo za kufuatilia hali ya wakimbizi wa nchini Libya.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu William Swing, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Wakimbizi, Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad al Hussein, kamishna mwandamizi wa masuala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa  na Martin Kobler, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya wakisisitizia wajibu wa kufuatiliwa suala la wakimbizi wa liko nchini humo. Maafisa hao walitoa mwito huo katika kikao chao kilichofanyika jana mjini Geneva Uswisi.

Wakati huo huo Shirika la Kimataifa la Wakimbizi, leo limetoa tamko likiitaka jamii ya kimataifa kuwa kitu kimoja katika kukabiliana na mgogoro wa hivi sasa wa Libya na kuwa mstari wa mbele katika kulinda haki za wakimbizi nchini humo.

Mamia ya wahajiri haramu hupoteza maisha yao katika bahari ya Mediterranean wakati wanapojaribu kukimbilia Ulaya kupitia Libya. 

 

Libya imekumbwa na machafuko ya mtawalia tangu mwaka 2011 wakati shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO lilipoingilia kati na kuipindua serikali ya Kanali Muammar Gaddafi na baadaye kuitelekeza nchi hiyo huku silaha zikiwa zimetapakaa ovyo mikononi mwa watu.

Nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika imegeuka kuwa kituo kikuu cha magendo ya kila namna yakiwemo ya binadamu.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, karibu wakimbizi 230 wameshapoteza maisha tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2017 wakati wakijaribu kukimbilia barani Ulaya kupitia Libya.