Maelfu ya Wagambia wajitokeza kwa wingi kumuunga mkono Rais Barrow
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25332-maelfu_ya_wagambia_wajitokeza_kwa_wingi_kumuunga_mkono_rais_barrow
Maelfu ya raia wa Gambia wamejitokeza kwa wingi katika kongamano kubwa lililofanyika jana katika mji mkuu wa nchi hiyo Banjul katika kumuunga mkono Rais Adama Barrow wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 18, 2017 23:12 UTC
  • Maelfu ya Wagambia wajitokeza kwa wingi kumuunga mkono Rais Barrow

Maelfu ya raia wa Gambia wamejitokeza kwa wingi katika kongamano kubwa lililofanyika jana katika mji mkuu wa nchi hiyo Banjul katika kumuunga mkono Rais Adama Barrow wa nchi hiyo.

Wagambia wametangaza uungaji wao mkono kwa rais huyo, kupitia mkusanyiko mkubwa katika uwanja wa michezo wa Uhuru uliopo eneo la Bakau, magharibi mwa mji wa Banjul, ambapo walitoa nara katika kumuunga mkono rais huyo. Katika kongamano hilo, viongozi na wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa nchi kadhaa za Kiafrika walihudhuria.

Raia wa Gambia wakionyesha uungaji wao mkono kwa Adama Barrow

Kadhalika raia wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika walilalamikia kitendo cha polisi kuwazuia kuingia kwenye uwanja huo wa Uhuru na badala yake kuwaruhusu wanadiplomasia wa Marekani na Uingereza, suala ambalo liliwakasirisha mno. Tarehe 18 Februari inakumbushia siku ambayo Gambia ilijipatia uhuru kutoka mikononi mwa Uingereza na siku hiyo hutambulika kwa jina la 'Siku ya Kuzaliwa mara ya tatu kwa nchi hiyo' kutokana na kumuondoa madarakani Yahya Jammeh, rais wa zamani wa nchi hiyo.

Sehemu ya furaha za wananchi

Jammeh aliyetawala Gambia kwa miaka 22 alishindwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika Disemba Mosi mwaka jana ambapo awali alikubali matokeo hayo. Hata hivyo baadaye  alibadili msimamo wake huo na kuyakana matokeo hayo na hivyo kujikuta anakabiliwa na mashinikizo ya kimataifa. 

Hatimaye Jammeh alikubali kungátuka madarakani  na hivi sasa yuko uhamishoni nchini Guinea ya Ikweta…/