Hilali Nyekundu: Wahajiri 74 wafa maji pwani ya Libya wakielekea Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25450-hilali_nyekundu_wahajiri_74_wafa_maji_pwani_ya_libya_wakielekea_ulaya
Shirika la Hilala Nyekundu la Libya limesema makumi ya wahajiri wamekufa maji katika Bahari ya Mediterranean wakijaribu kuelekea barani Ulaya.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Feb 21, 2017 10:25 UTC
  • Hilali Nyekundu: Wahajiri 74 wafa maji pwani ya Libya wakielekea Ulaya

Shirika la Hilala Nyekundu la Libya limesema makumi ya wahajiri wamekufa maji katika Bahari ya Mediterranean wakijaribu kuelekea barani Ulaya.

Mohammed al-Misrati, Msemaji wa shirika hilo ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, timu za waokoaji na wapiga mbizi mapema leo Jumanne zimegundua miili 74 katika pwani ya Libya, katika mji wa Zawiya, kusini magharibi mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Hata hivyo amesema wameanzisha uchunguzi kubaini kiini cha kufa maji wahajiri hao na kuongeza kuwa miili yao  imepelekwa mji mkuu Tripoli kwa ajili ya shughuli za kutambuliwa na kuzikwa.

Miili ya wahajiri ikiopelewa kutoka baharini

Mapema mwezi huu wa Februari, vikosi vya doria katika pwani ya Italia vilitangaza kuwa vimewaokoa wahajiri 1,300 katika bahari ya Mediterania.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, karibu wakimbizi 300 wameshapoteza maisha tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2017 wakati wakijaribu kukimbilia barani Ulaya kupitia Libya. 

Wahajiri 181,000 waliwasili nchini Italia mwaka jana kupitia bahari ya Mediterania, akthari yao wakiwa wameondokea nchini Libya. Mashirika ya misaada yanakadiria watu zaidi ya 5,000 walifariki dunia mwaka uliomalizika wa 2016 katika jitihada za kuingia barani Ulaya