Wahajiri wa Kiafrika wazidi kufa maji wakielea Ulaya
Makumi ya wahajiri wa Kiafrika wanahofiwa kufa maji katika Bahari ya Mediterranean wakijaribu kuelekea barani Ulaya.
Msemaji wa Gadi ya Pwani ya Libya, Ayoub Gassim, ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba, wanahofia wahajiri 25 wamekufa maji baada ya boti yao kuzama katika Bahari ya Mediterranean. Amesema boti hiyo iliondoka wilaya ya Tajoura, viungani mwa mji mkuu Tripoli saa saba usiku na kisha ikaanza kupiga king'ora cha usaidizi mwendo wa saa saba mchana.
Gassim amesema timu za waokoaji zimefanikiwa kunusuru wahajiri 115 wakiwemo wanawake sita, kati ya 140 waliokuwa katika boti hiyo; na kufikisha idadi ya wahamiaji wa Kiafrika waliookolewa wakijaribu kuelekea Ulaya kufikia 2000 tangu Januari mwaka huu.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Mohammed al-Misrati, Msemaji wa shirika la Hilali Nyekundu la Libya alisema wapiga mbizi waligundua miili 74 katika pwani ya Libya, katika mji wa Zawiya, kusini magharibi mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, zaidi ya wakimbizi 300 wameshapoteza maisha tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2017 wakati wakijaribu kukimbilia barani Ulaya kupitia Libya. Kwa mujibu wa Shirika la Uhamiaji Dunia IOM, zaidi ya wahajiri 5,000 walifariki dunia katika Bahari ya Mediterranean mwaka uliomalizika wa 2016 katika jitihada za kuingia barani Ulaya