Wanajeshi waliopanga mapinduzi dhidi ya Jammeh wajiunga na jeshi la Gambia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25976-wanajeshi_waliopanga_mapinduzi_dhidi_ya_jammeh_wajiunga_na_jeshi_la_gambia
Rais Adama Barrow wa Gambia amekubali kujiunga na jeshi wanajeshi wa zamani waliotuhumiwa kupanga mapinduzi dhidi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Yahya Jammeh.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 05, 2017 12:57 UTC
  • Wanajeshi waliopanga mapinduzi dhidi ya Jammeh wajiunga na jeshi la Gambia

Rais Adama Barrow wa Gambia amekubali kujiunga na jeshi wanajeshi wa zamani waliotuhumiwa kupanga mapinduzi dhidi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Yahya Jammeh.

Rais Adama Barrow amekubali kujiunga na jeshi la nchi hiyo wanajeshi sita wa zamani wanaotuhumiwa kupanga njama ya kumpindua Rais wa zamani wa nchi hiyo Yahya Jammeh. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wanajeshi hao  sita tayari wameanza kazi katika jeshi la Gambia. Itakumbukwa kuwa idadi kadhaa ya wanajeshi wa Gambia  mwaka 2014 walipanga njama ya kutaka kumpindua Rais wa zamani wa nchi hiyo Yahya Jammeh; njama ambayo iligonga mwamba.

Rais wa zamani wa Gambia, Yahya Jammeh ambaye alinusurika kupinduliwa madarakani mwaka 2014 

Katika utawala wake wa miaka 22 huko Gambia, Yahya Jammeh alinusurika mara kadhaa kung'olewa madarakani katika njama tofauti za mapinduzi zilizotekelezwa dhidi yake, na njama hatari zaidi ilikuwa hiyo ya mwaka 2014 ambapo wanajeshi hao walijaribu kuidhibiti ikulu ya Rais wakati Jammeh mwenyewe akiwa nje ya nchi. Rais mpya wa Gambia Adama Barrow, mwezi uliopita alitoa msamaha kwa wanajeshi hao waliopanga njama ya mapinduzi dhidi ya Jammeh. Itakumbukwa kuwa, mwezi Aprili mwaka 2015 mahakama ya kijeshi ya Gambia iliwapata na hatia wanajeshi wote sita waliopanga kumpindua Jammeh, huku watatu kati yao wakihukumiwa kifo.