Jeshi la Libya lashambulia maeneo ya al Qaida
Jeshi la Libya limefanya mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo ya kundi la kigaidi la al Qaida katika eneo lenye mafuta mengi linalojulikana kwa jina la "Hilali ya Mafuta" kaskazini mwa nchi hiyo.
Televisheni ya Sky News imetangaza habari hiyo na kuzinukuu duru za kijeshi za Libya upande wa mashariki zikitangaza kuwa, jeshi la anga la nchi hiyo limeshambulia magari 25 ya deraya ya kundi la kigaidi linalojiita Brigedi za Ulinzi wa Benghazi, tawi la mtandao wa kigaidi wa al Qaida, kusini mwa eneo la Bin Jawad, mashariki mwa Sirte.
Jeshi la Libya la mashariki mwa nchi hiyo linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar limeanzisha opereseheni kubwa za kijeshi tangu wiki iliyopita kwa shabaha ya kukomboa vijiji vinavyodhibitiwa na kundi hilo la kigaidi.

Hivi karibuni brigedi hizo zililiteka eneo la Ras Lanuf, magharibi mwa Ajdabiya kabla ya kuyateka maeneo ya bin Jawad na al Sidra ambayo ndiyo yenye bandari kubwa zaidi za mafuta nchini Libya. Maeneo hayo matatu yanajulikana kwa jina la Hilali ya Mafuta na yako katika fukwe za nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Jeshi la Libya upande wa mashariki mwa nchi hiyo, mwezi Septemba mwaka jana lilifanikiwa kuwafurusha wanamgambo wa al Qaida na kulikomboa eneo la Ras Lanuf.
Wakati huo huo Brigedia Jenerali Muhammad al Manfur, kamanda wa kitengo cha operesheni cha jeshi la anga la Libya jana alikanusha madai ya kuweko askari wa Russia mashariki mwa nchi hiyo, na kusema kuwa, hakuna askari yeyote wa Russia katika sehemu yoyote ile ya Libya.