Mar 14, 2017 14:57 UTC
  • Serikali ya Sudan Kusini yataka Machar atambuliwe kama gaidi

Serikali ya Sudan Kusini imezitaka nchi za eneo kumtambua Riek Machar, aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo kama gaidi, baada ya askari watiifu kwa kiongozi huyo kuwateka nyara wafanyakazi wawili wa kigeni, na kuitisha kikomboleo ili wawaachie huru.

Michael Makuei, Waziri wa Habari wa Sudan Kusini amewaambia waandishi wa habari mjini Juba kuwa, wapiganaji watiifu kwa Machar waliwateka nyara Ambrose Edward na Midhum Ganesh raia wa India wanaofanya kazi katika shirika moja la utoaji misaada ya kibinadamu katika eneo la Upper Nile Jumatano iliyopita, na wameitaka serikali ya Juba iwape dola milioni 1 kama kikomboleo ili wawaachie huru.

Makuei amesema kitendo hicho kinadhihirisha kuwa, Machar anaongoza harakati na magenge ya kigaidi katika hiyo changa zaidi barani Afrika na kwa msingo huo, viongozi wa kieneo hawafai kumpa hifadhi, kufanya mashauriano naye wala kumheshimu.

Sehemu kidogo ya Wasudan Kusini walioathiriwa na mgogoro wa kisiasa uliopo

Huku hayo yakiarifiwa, Umoja wa Mataifa umekosoa hatua ya serikali ya Sudan Kusini kuongeza malipo ya viza ya kazi kwa kiwango kikubwa kwa raia wa kigeni wanaofanya kazi nchini humo.

Guiomar Pau Sole, Msemaji wa Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya umoja huo OCHA amesema kuwa, mashirika ya utoaji misaada hayafai kutozwa kiasi kikubwa hicho kama ada ya viza haswa kwa kutilia maanani kuwa, watu milioni 5.5 sawa na nusu ya watu wa nchi hiyo wanahitaji misaada ya kibinadamu kama vile chakula na matibabu. 

Hivi karibuni, Waziri wa Habari wa Sudan Kusini Michael Makuei alitangaza kuwa, serikali ya Juba itatoza gharama ya viza ya kazi kati ya dola 1000 hadi 10,000 za Marekani kwa raia wa kigeni wanaofanya kazi nchini humo kwa mwaka, kutoka dola 100.

Tags