Gambia kuunda tume ya ukweli na maridhiano
(last modified Fri, 24 Mar 2017 04:31:06 GMT )
Mar 24, 2017 04:31 UTC
  • Gambia kuunda tume ya ukweli na maridhiano

Serikali ya Gambia imetangaza kuwa itaunda tume ya ukweli na maridhiano na kuwalipa fidia waathirika wa jinai zilizofanywa na serikali ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Yahya Jammeh inayotuhumiwa kuwatesa na kuwaua watu walioshukiwa kuwa wapinzani wa serikali hiyo.

Waziri wa Sheria wa Gambia Abubacarr Tambadou amesema kupitia taarifa kuwa serikali itachunguza pia fedha za Jammeh aliyekimbilia uhamishoni Guinea ya Ikweta mwezi Januari baada ya kufikia kikomo utawala wake ulioanzia mwaka 1994 alipotwaa madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi.

Tambadou amefafanua kuwa tume hiyo ya ukweli na maridhiano itakayozingatia pia kuwalipa fidia waathirika itaundwa katika kipindi cha miezi sita ijayo na vikao vya kupokea na kusikiliza maoni ya wananchi vinategemewa kuanza mwishoni mwa mwaka huu.

Rais Adama Barrow wa Gambia

Tangu serikali mpya ya Rais Adama Barrow iingie madarakani nchini Gambia imechukua hatua kadhaa za kurejesha utawala wa sheria na kuimarisha vyombo vya mahakama.

Serikali ya Banjul inakusudia kutafiti kwanza tume za aina hiyo zilizoundwa katika mataifa mengine. Itakumbukwa kuwa Afrika Kusini iliunda Tume ya Ukweli na Maridhiano baada ya kutokomezwa mfumo wa utawala wa ubaguzi wa rangi wa Apatheidi nchini humo; hatua ambayo iliingwa na mataifa mengine kadhaa ya Kiafrika.

Lengo la tume hiyo ni kuwashajiisha watu kuungama jinai walizofanya katika serikali iliyopita na pia waathirika wa jinai hizo kuweka hadharani uonevu na mateso yaliyowapata…/