Maharamia wa Somalia wateka nyara meli ili kuitumia kuendeshea mashambulizi
(last modified Fri, 24 Mar 2017 15:20:21 GMT )
Mar 24, 2017 15:20 UTC
  • Maharamia wa Somalia wateka nyara meli ili kuitumia kuendeshea mashambulizi

Maharamia wameteka nyara meli moja ya uvuvi ya Somalia ili kuitumia kama kituo cha kuendeshea mashambulizi dhidi ya meli kubwa. Hayo yameelezwa leo na polisi ya Somalia wiki moja baada ya maharamia wa nchi hiyo kuteka nyara meli ya kwanza ya kibiashara tangu mwaka 2012.

Maafisa wa Somalia wamesema kuwa, mabaharia kumi wa Yemen waliokuwa ndani ya meli hiyo wametelekezwa katika eneo la pwani. Mkuu wa Kikosi cha Jeshi la Majini cha Polisi katika eneo la Puntland, Abdirahman Mohamud amesema kuwa maharamia hao wameiteka nyara meli ya uvuvi ya Somalia lengo likiwa ni kuitumia kuziteka nyara meli kubwa baharini.

Maharamia wa Somalia 

Ameongeza kuwa maharamia hao wamewatelekeza mabaharia kumi wa Yemen na mlinzi mmoja wa Kisomali katika eneo la pwani na kutoweka na meli hiyo ya uvuvi pamoja na chakula, jiko, nahodha na mhandisi.  

Hili ni shambulio la pili kuwahi kufanywa na maharamia wa Somalia mwezi huu. Tarehe 13 mwezi huu maharamia wa Somalia waliiteka nyara meli moja ndogo ya mafuta katika eneo hilo hilo. Maharamia waliohusika katika utekaji nyara wa leo hawana lengo la kuishikilia meli hiyo na wafanyakazi wake ili walipe fidia, bali wanataka kuitumia kama kituo chao cha kuzishambulia meli kubwa.

Tags