Maafisa usalama wa Afrika watahadharisha kuhusu hatari ya makundi ya kigaidi
Maafisa wa upelelezi na vyombo vya usalama wa nchi 30 za Afrika walioshiriki katika mkutano wa amani nchini Sudan wametahadharisha kuhusu vitisho vya makundi ya kigaidi barani humo.
Maafisa hao wamesema makundi ya kigaidi hususan Daesh yameelekeza harakati zao katika nchi za Afrika, na wametilia mkazo udharura wa kuanzishwa kambi moja ya kupambana na ugaidi.
Washiriki katika mkutano huo pia wamesema, kujiunga kwa vijana wengi wa Afrika na makundi ya kigaidi ni tishio kubwa kwa nchi za bara hilo. Maafisa hao wa taasisi za upelelezi na usalama wa nchi 30 za Afrika wamesema kuwa, asilimia 20 hadi 40 ya vijana wa Kiafrika waliokuwa katika safu za magaidi katika nchi za Syria na Iraq wamerejea katika nchi zao na kwamba, suala hilo ni hatari kubwa kwa bara zima la Afrika.
Mkutano wa amani wa nchi za Afrika ulioanza Jumatatu iliyopita katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum ulimaliza shuguli zake jana usiku.