Kuendelea mgogoro wa Libya na hatari ya kugawanywa nchi hiyo
Mshauri wa Rais wa Marekani ametoa pendekezo la kugawanywa nchi ya Libya katika nchi tatu zinazojitawala. Pendekezo hilo limetolewa katika kipindi hiki ambapo Libya inaendelea kuzongwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa.
Sebastian Gorka ambaye ni mshauri wa Rais Donald Trump wa Marekani amesema Libya inaweza kugawanywa katika sehemu tatu zenye makao makuu katika mikoa ya Brega (kaskazini mashariki), Tripoli na Fezzan (kusini magharibi).
Wiki kadhaa kabla ya kuteuliwa na Donald Trump kuwa mshauri wake katika masuala ya siasa za nje, Gorka alikutana na wanadiplomasia wa nchi za Ulaya na kuwaeleza mpango huo wa kuigawa Libya katika nchi tatu zinazojitawala.
Mpango huo wa Sebastian Gorka umetolewa katika hali ambayo Libya imekuwa katika ghasia na machafuko ya ndani tangu Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) lilipoparamia mawimbi ya malalamiko ya wananchi na dhidi ya kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi na kumuondoa madarakani hapo mwaka 2011. Japokuwa mapatano ya makundi mbalimbali ya Libya yaliyotiwa saini Skheirat nchini Moroco mwaka 2015 yalileta matumaini ya kukomeshwa ghasia na mgogoro wa kisiasa wa Libya, lakini serikali iliyoundwa baada ya makubaliano hayo imeshindwa kufanya lolote kutokana na kutotambuliwa na baadhi ya makundi yanayobeba silaha na kutopasishwa na bunge la nchi hiyo. Suala hilo limeifanya Libya iendelee kukumbwa na vita na mapigano ya ndani na kudhibitiwa na makundi tofauti yakiwemo baadhi ya maeneo yanayodhibitiwa na kundi la kiwahabi na kitakfiri la Daesh.
Hayo yote yanaendelea huku nchi nyingi za Magharibi zikiendelea kuikodolea macho ya tamaa Libya kutokana na nafasi yake ya kistratijia na utajiri wake mkubwa wa mafuta. Utajiri huo mkubwa wa mafuta unaifanya Libya kuwa medani ya ushindani wa nchi kubwa zinazotumia makundi hasimu kwa ajili ya kuwa na ushawishi nchini humo, huku makundi ya kigaidi kama Daesh yakitumia fursa hiyo kujiimarisha zaidi. Makundi haya ya kigaidi yamekuwa yakiteka na kudhibiti visima na taasisi za mafuta za Libya kwa ajili ya kuzidisha pato lao. Japokuwa maeneo mengi ya mafuta yamekombolewa na jeshi la Libya kutoka kwenye makucha ya makundi ya kigaidi, lakini suala hilo la kugombania udhibiti wa visima na maeneo ya mafuta lingali linazusha vita na mapigano ya ndani.
Katika upande mwingine tangu mwanzoni mwa mgogoro wa Libya nchi nyingi za Ulaya zimekuwa zikiingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo kwa njia moja au nyingine na kukwamisha jitihada za kurejeshwa amani na utulivu nchini humo kutokana na kwamba, kila moja kati ya nchi hizo inafuatilia maslahi yake makhsusi. Vivyo hivyo baadhi ya nchi za Kiarabu ambazo zimekuwa zikiyasaidia na kuyaunga mkono makundi hasimu kwa ajili ya kutaka kuwa na ushawishi nchini Libya. Misaada hii ya kifedha na kijeshi baadhi ya nchi za Kiarabu inachochea zaidi moto wa vita na migawanyiko nchini Libya.
Japokuwa kwa muda sasa wataalamu wa masuala ya siasa wamekuwa wakitahadharisha kuhusu suala la kugawanywa nchi Libya kutokana na njama zinazofanywa na baadhi ya madola ya kigeni yanayokodolea macho utajiri wa nchi hiyo, lakini sasa na baada ya kutangazwa wazi mpango wa Marekani wa kutaka kuigawa nchi hiyo katika sehemu tatu zinazojitawala, viongozi wa makundi mbalimbali ya nchi hiyo hawana budi isipokuwa kuamka kutoka kwenye usingizi na kuzuia njama hizo chafu kwa kurejea katika meza ya mazungumzo. Kwa hakika kutangazwa mpango huo wa Marekani ni kengele ya hatari kwa wanasiasa, makundi na watu wenye ushawishi katika jamii ya Libya kwa ajili ya kutafuta njia ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo na kuokoa nchi yao isitumbukie katika mikono ya wakoloni mamboleo.