UN: Wahajiri wa Kiafrika wanauzwa kati ya dola 200 na 500
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27630-un_wahajiri_wa_kiafrika_wanauzwa_kati_ya_dola_200_na_500
Wakala wa wahamiaji wa Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake kutokana kile kinachoonekana ni kurejea kwa biashara ya utumwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 11, 2017 10:54 UTC
  • UN: Wahajiri wa Kiafrika wanauzwa kati ya dola 200 na 500

Wakala wa wahamiaji wa Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake kutokana kile kinachoonekana ni kurejea kwa biashara ya utumwa.

Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM) tawi la Libya limewaambia waandishi wa habari mjini Geneva nchini Uswisi kuwa, wahajiri wa Kiafrika wanauzwa kati ya dola 200 na 500 za Marekani, ambapo wanaowanunua wanaenda kuwatumia kama vyombo vya kukidhi mahitaji ya ngono huku wengine wakifanyishwa kazi za sulubu.

Othman Belbeisi, Mkuu wa IOM tawi la Libya ameongeza kuwa, baadhi ya wahajiri hao wa Kiafrika wanatumiwa katika ujenzi wa miradi mbalimbali na kazi za shambani bila malipo wanakouzwa.

Afisa huyo wa Shirika la Kimataifa la Wahajiri la Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa, aghalabu ya wahajiri hao wanatoka katika nchi za Nigeria, Senegal na Gambia na wamekuwa wakienda Libya kwa ajili kutaka kupelekwa katika nchi za Ulaya kupitia safari hatari ya baharini.

Wahajiri wa Kiafrika wakijaribu kuelekea Ulaya

Belbesi ameongeza kuwa, akthari ya wahajiri wa Kiafrika waliozungumza na IOM wamesema baadhi yao wamekuwa wakinunuliwa na kufanyishwa kazi ngumu bila malipo katika makarakana na maegesho ya gari, katika wa kusini wa Sabha, moja ya vitovu vya magendo ya binadamu nchini Libya. Amesema wahajiri wanawake wanabakwa kiholela huku baadhi yao wakilazimika kuingilia biashara ya ukahaba.

Wiki iliyopita, watu wanne wanaotuhumiwa kufanya magendo ya binadamu waliuawa katika makabiliano na askari wa Gadi ya Pwani ya Libya, siku chache baada ya maafisa wa gadi hiyo kuwatia nguvuni wahajiri haramu 60 wenye uraia wa Bangladesh ambao walikuwa wanajaribu kuelekea barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranean.