Libya yaituhumu EU kuwa imekataa kutekeleza ahadi zake kuhusu wahajiri
Waziri Mkuu wa serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ameukosoa Umoja wa Ulaya (EU) kwa kukataa kutekeleza ahadi ulizozitoa kuhusu kuipatia ufumbuzi kadhia ya magendo wa wahajiri.
Tovuti ya habari ya Russia Today imenukuu matamshi ya Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu wa Libya ambaye amenukuliwa na gazeti la Ujerumani la Bild akiikosoa vikali EU kwa kufeli kutekeleza ahadi zake, akisisitiza kuwa "Umoja wa Ulaya haujatusaidi kwa chochote, ulitoa ahadi hewa tu".
Sarraj ameonya kuwa, iwapo Libya haitapokea misaada ya EU kwa ajili ya kukabiliana na wimbi la wahajiri, basi nchi za Ulaya zijiandae kupokea wahajiri zaidi karibuni hivi.
Kadhalika amesisitizia umuhimu wa Umoja wa Ulaya kutekeleza pia ahadi uliyoitoa ya kutuma timu ya wataalamu wa kusaidia kulinda pwani ya Libya, inayotumiwa na wanaofanya biashara haramu ya magendo ya binadamu.
Hapo jana, Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM) tawi la Libya liliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva nchini Uswisi kuwa, wahajiri wa Kiafrika wanauzwa kati ya dola 200 na 500 za Marekani, ambapo wanaowanunua wanaenda kuwatumia kama vyombo vya kukidhi mahitaji ya ngono huku wengine wakifanyishwa kazi za sulubu.
Wimbi la uhajiri hususan la vijana kuelekea nchi za Ulaya limeendelea kuongezeka siku hadi siku kupitia usafiri hatarishi wa bahari ya Mediterania.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhajiri (IOM), zaidi ya watu 6,000 wameokolewa mnamo siku chache zilizopita katika bahari hiyo wakitoka Libya kuelekea Italia. Wahamiaji 16,248 tayari wamewasili nchini Italia mwaka huu ikiwa ni idadi kubwa zaidi kulinganisha na 13,825 waliowasili katika kipindi sawa na hicho mwaka uliopita