Waislamu waliouawa na jeshi la Nigeria wakumbukwa katika 'Siku ya Mashahidi'
Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria imeadhimisha siku ya mashahidi katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na wananchi, jamaa wa familia za mashahidi, wasomi wa kidini na shakhsia mbalimbali wakubwa wa nchi hiyo. Washiriki katika maadhimisho hayo, walibeba picha za mashahidi hao wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ili kuwakumbuka, mashahidi ambao waliuawa kwa dhulma na askari wa serikali ya nchi hiyo bila kosa lolote.
Marasimu ya kuwakumbuka mashahidi yamefanyika katika maeneo tofauti ya Nigeria katika hali ambayo hivi karibuni pia Waislamu wa nchi hiyo wakishirikiana na Wakristo walifanya maandamano ya kumuunga mkono Sheikh Ibrahim Yaqoub El Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria na kuitaka serikali imuachilie huru. Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya mahakama ya Nigeria, maandalizi ya kuachiliwa huru kiongozi huyo wa Kiislamu pamoja na mke wake, yalikamilika yapata miezi mitatu iliyopita, lakini pamoja na hayo bado serikali ya Rais Muhammadu Buhari imeendelea kumzuilia shakhsia huyo. Askari wa Nigeria walivamia Husseiniyyah ya Waislamu wa Shia ya Baqiyatullah katika mji wa Zaria, mkoa wa Kaduna hapo mwezi Disemba mwaka 2015.
Katika shambulizi hilo askari hao mbali na kuua mamia ya Waislamu, walimtia nguvuni Sheikh Ibrahim Yaqoub El Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria. Kadhalika askari hao wakatili walimtia mbaroni mke wa kiongozi huyo pamoja na makumi ya Waislamu wa Kishia. Baada ya uvamizi huo, serikali ya Nigeria ilishadidisha ukatili na ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Shia nchini humo.