Apr 27, 2017 04:33 UTC
  • Rais wa Angola aafiki uchaguzi mkuu ufanyike Agosti 23

Rais Jose Eduardo dos Santos wa Angola amesaini dikrii inayoruhusu tarehe 23 Agosti mwaka huu kuwa siku ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo.

Taarifa iliyotangazwa na idhaa ya serikali hapo jana imesema kuwa, uchaguzi mkuu utafanyika Agosti 23, ambapo Dos Santos anatazamiwa kuachia ngazi baada ya kuwa rais wa nchi hiyo kwa karibu miongo minne.

Hata hivyo taarifa hiyo imesisitiza kuwa, Dos Santos ambaye ameiongoza nchi hiyo ya Kiafrika yenye utajiri wa mafuta ghafi atasalia kuwa kinara wa chama tawala cha MPLA.

Angola ni mzalishaji namba 2 wa mafuta ghafi Afrika, na uchumi mkubwa wa 3 barani humo

Uamuzi huu wa Dos Santos unajiri chini ya saa 48 baada ya Baraza la Uongozi la Rais wa Angola ambalo hutoa ushauri kuhusu maamuzi ya nchi kupendekeza tarehe 23 Agosti kuwa siku ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini.

Itakumbukwa kuwa, chama tawala nchini Angola cha MPLA mwezi Disemba mwaka jana kilimchagua Joao Lourenco mwenye umri wa miaka 63 kuwa mgombea wa kiti cha urais wa chama hicho.

Jose dos Santos aliye na umri wa miaka 74 ni kiongozi wa pili barani Afrika aliyesalia madarakani kwa muda mrefu zaidi, na mwezi Februari mwaka huu alisema kuwa hatagombea tena kiti cha urais katika uchaguzi ujao.

Tags