UN yatuma misaada kwa raia wa Kongo DR nchini Angola
Umoja wa Mataifa umelazimika kutumia usafiri wa ndege kutuma misaada yake ya kibinadamu kwa makumi ya maelfu ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walioko nchini Angola.
Sharon Cooper, Mjumbe wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR katika eneo la kusini mwa Afrika ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, asasi hiyo imetuma shehena ya kwanza ya misaada kwa ajili ya raia 11,000 wa Kongo DR, walioko katika eneo la Dundo, yapata kilomita 100 kaskazini mwa mpaka wa DRC na Angola.
Amesema msaada huo unajumuisha vyakula, vyandarua, mablanketi na mahitaji mengineyo na kwamba karibuni hivi shirika hilo litatuma misaada zaidi nchini Angola, kwa ajili ya raia wa Kongo DR wanaotafuta hifadhi baada ya kukimbia machafuko nchini kwao.
Zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuhama makwao kufuatia miezi minane ya machafuko yanayozidi kusambaa katika majimbo ya Kasai, Lomami na Sankuru, kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura, OCHA imesema, Umoja wa Mataifa na wadau wake wamezindua ombi la dola milioni 64.5 ili kushughulikia mahitaji ya dharura ya kibinadamu ya watu 731,000 walioathiriwa na mzozo huo kwa kipindi cha miezi sita ijayo. OCHA imesema idadi ya watu waliolazimika kuhama makwao ni kubwa sana katika mikoa mitano yenye idadi ya watu wapatao milioni 25.