UN: Watoto milioni 2 wa Sudan Kusiniwamelazimika kuwa wakimbizi
Umoja wa Mataifa umesema watoto zaidi ya milioni 2 wa Sudan Kusini wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano na ukame vinavyoisakama nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Valentin Tapsoba, Mkuu wa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR barani Afrika amesema watoto milioni moja wa Sudan Kusini wamelazimika kuwa wakimbizi nje ya nchi huku wengine zaidi ya milioni moja wakiyahama makazi yao na kuwa wakimbizi wa ndani.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, kati ya watoto wanne, watatu miongoni mwao hawaendi shule. Kadhalika takwimu za UN zimebainisha kuwa, zaidi ya watoto 1000 wameuawa hadi kufikia sasa kutokana na machafuko, mapigano na baa la njaa linaloendelea kushuhudiwa nchini Sudan Kusini.
Uganda, hadi sasa imeshapokea wakimbizi zaidi ya 832,000 kutoka Sudan Kusini wakiwemo zaidi ya 270,000 walioko kwenye kambi ya Bidibidi, huku Sudan akisema kuwa karibu kila siku wakimbizi 1500 raia wa Sudan Kusini huingia nchini humo. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu 2017, inakadiriwa jumla ya wakimbizi laki moja na elfu 80 wa Sudan Kusini wataingia nchini Sudan.
Sudan Kusini ilitumbukia katika mgogo wa kisiasa mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu aliyekuwa makamu wake wa rais kwamba alikula njama ya kutaka kumpindua madarakani.