Iran kufungua kampuni ya kutengeneza trekta nchini Zimbabwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29060-iran_kufungua_kampuni_ya_kutengeneza_trekta_nchini_zimbabwe
Balozi wa Iran mjini Harare amesema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kuanzisha kampuni ya kutengeneza tingatinga nchini Zimbabwe.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 14, 2017 02:48 UTC
  • Iran kufungua kampuni ya kutengeneza trekta nchini Zimbabwe

Balozi wa Iran mjini Harare amesema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kuanzisha kampuni ya kutengeneza tingatinga nchini Zimbabwe.

Ahmad Erfanian, balozi wa Iran mjini Harare aliyasema hayo jana Jumamosi alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa na kufafanua kuwa, nchi mbili hizi zimesaini makubaliano ya ushirikiano, ambapo Tehran imekubali kuiuzia Zimbabwe trekta zake kwa kufungua kampuni ya kutengeneza tingatinga nchini humo.

Kadhalika pande mbili hizo zimekubaliana kuongezwa kiwango cha mabadilishano ya kiuchumi na kibiashara baina ya nchi mbili hususan katika nyuga za sayansi, teknolojia, elimu, uchimbaji madini na kilimo.

Sekta ya kilimo Zimbababwe itapigwa jeki na trekta za Iran

Balozi wa Iran mjini Harare amesema uhusiano wa nchi mbili hizi una historia ndefu haswa kwa kuzingatia kuwa marais wanne wa Iran wamewahi kuitembelea Zimbabwe kama ambavyo Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo ya Kiafrika amewahi pia kuitembelea Iran mara nne.

Aidha mwanadiplomasia huyo wa Iran amebainisha kuwa, uhusiano mzuri wa kisiasa uliopo baina ya Iran na Zimbabwe ni fursa nzuri ya kuongezwa kiwango cha mabadilishano ya kiuchumi na kibiashara baina ya nchi mbili kwa kutilia maanani kuwa, Tehran na Harare zilikuwa washirika na marafiki wa karibu hata katika kipindi cha vikwazo.