Sisitizo la kuondolewa vikwazo vya kuingiza silaha nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29124-sisitizo_la_kuondolewa_vikwazo_vya_kuingiza_silaha_nchini_libya
Katika mwendelezo wa mashauriano kwa lengo la kuimarisha usalama na uthabiti nchini Libya, Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri amekutana na kamanda mkuu wa jeshi la Libya na kusisitizia umuhimu wa kuondolewa vikwazo vya uingizaji silaha nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 15, 2017 09:01 UTC
  • Sisitizo la kuondolewa vikwazo vya kuingiza silaha nchini Libya

Katika mwendelezo wa mashauriano kwa lengo la kuimarisha usalama na uthabiti nchini Libya, Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri amekutana na kamanda mkuu wa jeshi la Libya na kusisitizia umuhimu wa kuondolewa vikwazo vya uingizaji silaha nchini humo.

Rais Al-Sisi aliyasema hayo katika mazungumzo na Jenerali Khalifa Haftar, kamanda mkuu wa jeshi la Libya huko Cairo, mji mkuu wa Misri ambapo sanjari na kuashiria juu ya suala la kuondolewa vikwazo hivyo alisema kuwa, haifai kutoa mwanya kwa pande za kigeni kuuchezea mustakabali wa taifa la Libya. Aidha mbali na kuashiria kwamba zana za jeshi la Libya ni sehemu ya mihimili ya jeshi hilo ya kutumika katika kupambana na ugaidi nchini, el Sisi amesisitizia pia msimamo thabiti wa Misri katika kufanya juhudi endelevu kwa lengo la kuupatia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa taifa hilo la kaskazini mwa Afrika kupitia njia ya kuyashawishi makundi hasimu kukaa kwenye meza ya mazungumzo.

Rais Al-Sisi na Jenerali Khalifa Haftar,

Libya ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa tangu mwaka 2011, kufuatia uingiliaji wa kijeshi wa Muungano wa Kijeshi wa NATO, uingiliaji ambao uliofuatiwa na kuondolewa madarakani aliyekuwa dikteta wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi. Maisha ya kijadi na kikabila, kutokuwa na uzoefu wa kidemokrasia, kuwepo maghala mengi ya silaha mikononi mwa makundi ya wanamgambo, uingiliaji wa nchi za Magharibi na baadhi ya nchi za eneo ndani ya taifa hilo, ni mambo ambayo yameendelea kuchochea moto wa vita nchini Libya kwa miaka kadhaa sasa.

Kanali Muammar Gaddafi, rais wa zamani wa Libya

Hali hiyo imesababisha makundi ya kigaidi hususan Daesh kukita mizizi ndani ya taifa hilo, ambapo licha ya jeshi la Libya kufanya juhudi kubwa kupambana nayo na kuyatimua makundi ya wanamgambo lakini hatari ya kuwepo tena makundi hayo imeendelea kutishia usalama wa nchi hiyo. Ni kwa sababu hiyo ndio maana katika kipindi cha wiki kadhaa za hivi karibuni yalitiwa saini makubaliano kadhaa baina ya viongozi wa Libya akiwemo rais wa serikali ya umoja wa kitaifa na Jenerali Khalifa Haftar ili kwa njia hiyo kuweza kuhitimisha mzozo unaoendelea nchini humo sambamba na kuandaliwa mazingira ya kufanyika uchaguzi ulio huru na wa haki. Ili kutekelezwa makubaliano hayo, kunahitajika pia mazungumzo endelevu baina ya pande husika.

Jeshi la Libya

Miongoni mwa nukta ambazo zimesisitizwa na viongozi wa Libya ni kuondolewa vikwazo vya silaha ilivyowekewa nchi hiyo. Hii sio mara ya kwanza kwa viongozi wa Libya kusisitizia juu ya umuhimu wa kuondolewa vikwazo vya kununua silaha. Hususan baada ya kuongezeka harakati za makundi ya kigaidi katika miji tofauti ya nchi hiyo, viongozi wa Libya wameongeza juhudi zao kutaka kuondolewa vikwazo hivyo. Kwa mujibu wa viongozi hao wa Libya, mapambano na makundi ya kigaidi yanahitajia silaha, ambapo silaha zilizopo nchini humo si tu hazitoshi, bali hata zile silaha muhimu ziko mikononi mwa makundi tofauti ya wanamgambo wenye kuendesha harakati za uasi nchini humo. Ni kwa msingi huo, ili kuimarisha jeshi la Libya hususan katika kupambana na ugaidi, kwanza kunahitaji kukarabatiwa mfumo wa zana za kijeshi kwa kuondolewa vikwazo vya silaha, ambako kutaisaidia sana serikali ya Tripoli kuweza kulikarabati jeshi lake na kupata nguvu kwa ajili ya kupambana na magenge hatari ya kigaidi nchini.

Wanamgambo wa Libya

Kabla ya hapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na katika uga huo wa kuondolewa vikwazo tajwa, liliitaka serikali ya umoja wa kitaifa kuandaa mazingira kwa ajili ya utekelezwaji wa suala hilo ili kwa njia hiyo kuzuia silaha hizo zisiyafikie makundi ya wanamgambo. Hii ni kwa kuwa pande zilizoiwekea vikwazo Libya zilitumia kisingizio kwamba ikiwa nchi hiyo itapewa fursa ya kununua silaha, suala hilo litaimarisha harakati za makundi ya wanamgambo nchini, hasa kwa kuzingatia kuwa hivi sasa Libya imegeuka kuwa moja ya njia kuu za misafara ya magendo ya silaha na soko kwa ajili ya mauzo ya bidhaa hiyo. Alaakulli hali, ili kumaliza mgogoro wa Libya kunahitajika ushirikiano wa nchi zote. Ni kwa ajili hiyo kuondolewa na kupunguzwa vikwazo vya silaha na kadhalika kuhitimishwa uingiliaji wa mambo ya ndani ya nchi hiyo unaofanywa na baadhi ya pande za kigeni na pia kumalizika uungaji mkono kwa makundi ya wanamgambo kunakofanywa na baadhi ya nchi, ni miongoni mwa hatua ambazo zitaisaidia Libya kuweza kufikia usalama na amani.